MKUU wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Albert Msando, ametatua mgogoro wa ardhi uliodumu kwa zaidi ya miaka 10 katika Mtaa wa Kambi 5 na Lukobe Juu Kata ya Lukobe Manispaa ya Morogoro ili kuhakikisha Wananchi walio na maeneo hayo wanapata hati za umiliki kwa mujibu wa sheria.
DC Msando, ametatua mgogoro huo katika mkutano wa hadhara wa utatuzi wa migogoro ya ardhi uliofanyika Februari 17/2022 kwenye Mitaa ya Kambi Tano na Lukobe Juu .
Akizungumza na Wananchi wa Mitaa hiyo,amesema kuwa kutokana na Mgogoro huo kati ya Wananchi hao na Chuo cha SUA ,ndio chanzo cha wananchi hao kukosa maendeleo kwa muda mrefu kutokana na kuwa na migogoro ya ardhi iliyodumu kwa muda mrefu.
Aidha, DC Msando, amesema kuwa wananchi wakitaka migogoro hiyo ya ardhi iishe, inaisha na pia wasipotaka migogoro iishe pia haiwezi kuisha.
“Leo tupo hapa kwa ajili ya utatuzi wa migogoro ya ardhi, hatuwezi kuwa na migogoro isiyoisha ambayo inachelewesha maendeleo najua wapo watu wachache ndio wanatuchelewesha katika mpango huu leo tungekuwa tunazungumzia maji, barabara, umeme, vituo vya afya lakini bado tupo katika migogoro haiwezekani, ni vyema kuchukua uamuzi wa kumaliza migogoro hiyo kwa wakati unaotakiwa ili kuweza kuleta maendeleo zaidi katika maeneo yetu, sitokuja tena hapa kwa ajili ya migogoro hii ndio mara yangu ya mwisho kinachofuata ni maamuzi tu" Amesema DC Msando.
"Nitoe rai, haya maeneo tunakwenda kuyapanga upya, sitosikia kuna biashara ya viwanja ikiendelea watakao fanya hivyo tutawachukulia hatua, tunataka kuupanga Mji huu, acheni kazi ifanyike, hakuna atakayebomolewa nyumba, wote mtapata haki zenu na kila mtu tutampa kiwanja hatutomuacha mtu nyuma, na hekari 43 za SUA tutawaachia wenyewe, na wale waliopo katika hekari hizo wanazohitaji SUA wataondoka huko ili tumalize mgogoro kabisa, na wenye hati kutoka Manispaa wasisumbuliwe, na wale waliosimamishwa ujenzi wakati wana hati waendelee, wavamizi wa maeneo ya wazi na barabara tutawachukulia hatua" Ameongeza DC Msando,.
Hata hivyo DC Msando, amesema kuwa mara baada ya Mkutano huo wa wananchi kuamua mpango wa kulipima upya eneo kuna hatua zitachukuliwa ikiwamo kupimwa kwa eneo lote la hekari 385 na kuwekewa bikoni, uhakiki wa watu wenye maeneo yao kwa wakulima na walionunua kila mtu atasimama katika eneo lake, Mipango Miji kuandaa mpango wa matumizi wa eneo hilo kwa kilichopo ardhini ili kupata maeneo ya huduma za kijamii na mpango huo kupelekwa Ofisi ya Kata , Kupimwa kwa Viwanja , mwisho hatua ya ugawaji wa hati za umiliki wa viwanja .
Amesema kuwa kila hatua zitakazofanyika watashirikisha wananchi ili waone kinachoendelea kuanzia hatua za mwanzo hadi za mwisho.
Naye, Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Ally Machela, amesema kuwa zoezi la upimaji litaendeshwa katika eneo husika na kila mtu atatakiwa kuwa katika eneo lake wakati wa uhakiki wa maeneo utakapoanza.
“Tutahamishia ofisi hapa, Wataalam wetu watakuwepo hapa ili kukamilisha zoezi la uhakiki hatua kwa hatua mpaka pale zoezi litakapo kamilika, hatuna lengo la kumpora mtu ardhi, sisi lengo letu ni kulinda ardhi ya wananchi kutoka kwenye ardhi ya maneno maneno na kuwa mali halali ambayo inaitwa hati, hii ni ardhi salama kwa manufaa ya wananchi na vizazi vyao vijavyo”Amesema Machela.
Nae mkazi wa mtaa wa Kambi 5, John Aizaki,amempongeza Mkuu wa Wilaya pamoja Uongozi wa Manispaa ya Morogoro katika kutatua mgogoro huo uliodumu muda mrefu huku akisema kuwa baada ya mgogoro huo wanaweza kuendeleza maeneo yao na kujiletea maendeleo.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa