Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Albert Msando, ametoa siku 21 kwa Uongozi wa Manispaa ya Morogoro , kuimarishwa kwa Kamati za ulinzi na usalama wa mtoto na wanawake katika ngazi za Kata ili zitumike kukabiliana na vitendo vya ukatili.
Kauli hiyo, ametoa Februari 07/2022 wakati wa Uzinduzi wa Kituo Cha Pamoja cha huduma ya mkono kwa mkono kwa watu waliofanyiwa ukatili (ONE STOP CENTRE) kilichopo katika Kituo cha afya cha Sabasaba Manispaa ya Morogoro.
Katika hatua nyingine, DC Msando, ametoa wito kwa mamlaka zinazosimamia kesi za ukatili dhidi ya watoto na wanawake kusimamia uharakishaji wa kesi hizo na waliotendewa vitendo vya ukatili waweze kupata haki zao.
"Shughulikieni kesi hizi za ukatili mapema, kesi hizi za ukatili zikiachwa muda mrefu zinapoteza ushahidi hivyo wahusika wanakosa haki zao zinazostahili na kuzidi kuathirika kisaikolojia na kufanya jitihada za kutokomeza vitendo hivyo kusuasua, hakikisheni mnazimaliza mapema na katika Kituo hiki fungueni majarada kwa wazazi wanaokwepa majukumu yao "Amesema DC Msando.
Naye Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro, Mhe. Pascal Kihanga, amewataka wazazi kushirikiana katika malezi na kuwajibika ili kuwalinda watoto kutofikia hatua ya kukinzana na Sheria.
Kwa upande wa Mkurugenzi wa Taasisi ya SAWA WANAWAKE TANZANIA, Bi. Hellen Nkarang'ango, amewaomba watakaosimamia Jengo hilo watoe huduma bora na kutimiza wajibu wao na kuzingatia ili kuweza kitimiza adhma ya ulinzi na usalama wa wanawake na watoto.
Bi. Hellen ,amesema kuwa Jengo hilo limejengwa kwa ufadhili wa J-Hope kwa kushirikiana na SAWA WANAWAKE TANZANIA, limegharimu kiasi cha shilingi Milioni 137 hadi kukamilika kwake ikijumuisha na samani zake.
Wakati huo huo, Mkurugenzi wa Mtandao wa Elimu Tanzania, Ochola Wayoga, amesema ipo haja kwa kamati zitakazoundwa kupatiwa mafunzo ya kutosha kwani malengo ya mafunzo hayo ni kuiwezesha kamati ya ulinzi na usalama wa mwanamke na mtoto kutekeleza vyema Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto ambao unalenga kusimamia haki na maendeleo ya mtoto na kuzuia ukatili dhidi ya mwanamke na mtoto na kuhakikisha wanapata haki zao na kutimiza wajibu wao vyema.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa