MKUU wa Wilaya ya Morogoro. Mhe. Bakari Msulwa, ameongoza mamia ya Wananchi wa Manispaa ya Morogoro ikiwamo Taasisi za Serikali na za watu binafsi kushiriki katika Kampeni ya Kupanda Miche ya Miti 150000 pembezoni mwa Bwawa la Mindu Manispaa ya Morogoro .
Zoezi hilo la Kampeni ya upandaji wa Miti pembezoni mwa Bwawa la Mindu Manispaa ya Morogoro limefanyika leo Desemba 09/2020 ikiwa ni Sherehe ya kutimiza miaka 59 ya Uhuru wa Tanzania.
Akizungumza na Viongozi mbalimbali pamoja na Wananchi walioshiriki katika zoezi hilo, DC Msulwa, amesema kuna umuhimu mkubwa na faida nyingi katika utunzaji wa mazingira hususani kupanda miti pembezoni mwa Mito na Mabwawa ambapo faida zake ni pamoja na kupata hewa safi, mvua za kutosha , kivuli, kutumika kama mipaka na kulinda vyanzo vya maji .
Aidha, amesema katika Siku ya leo , Wilaya yake ikiwamo Halmashauri zote mbili zimeandaa kampeni hiyo ya kupanda miti ili kulinda vyanzo vyake vya maji na kuendelea kutoa huduma bora ya Maji kwa Wananchi.
“Nimefurahishwa sana na Kampeni hii, kwani vyanzo vyetu vya maji hali tete watu wanafanya shghuli za kiuchumi katika vyanzo hivyo, wengine wanaziba vyanzo, sasa nimeambiwa Bwawa letu lina miaka 40, unafikiri kama tungeanza uharibifu nyuma tungekuwaje? Niwaombe tuache shughuli katika vyanzo vya maji, Bwawa lina jaa matope , tumeanza naomba wale wenye mashamba tuliyopanda miti watusaidie kusimamia miti hiyo ikue, ugomvi wetu utaanza hapa haiwezekani mazao yako yanakuwa na miti yetu inakufa wakati ipo katika shamba lake, nitoe wito tusiishie hapa kila mtu anawajibu wa kulinda vyanzo vya maji ili tuendelee kupata huduma hii” Amesema DC Msulwa.
“Pamoja na yote, nimefurahishwa sana na ujio wa wageni wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutoka Jimbo la Mwanakwerekwe Zanzibar, hii imeonyesha ni jinsi gani Muungano wetu ulivyo na thamani kubwa ndani ya Taifa hili, tunaomba tuuenzi Muungano wetu kwani unafaida kubwa sana kwa Taifa letu na Maendeleo yetu “ Ameongeza DC Msulwa.
Katika hatua nyingine, DC Msulwa, ametoa wito kwa Wazazi kuhakikisha ifikapo mwakani kila mzazi anapomwandishikisha mtoto na wale wanaoanza kidato cha kwanza kufika shuleni hapo akiwa na mche mmoja wa mti ili kuweka mazingira yenye ukijani.
Kwa upande wa Brigedia Jenerali , Mkuu wa Kikosi cha Jeshi la Mazao Kikosi cha Mzinga, Seif Hamisi, amewaasa washiriki na wananchi kujali mazingira ya sehemu wanazofanyia kazi na kuahidi kuwa miti hiyo iliyopandwa itatunzwa na kulindwa ipasavyo kwa kushirikiana na Uongozi na Wananchi wa eneo la Bwawa la Mindu ambapo ndipo Kambi ya Mzinga ilipo.
"Tunataka Kampeni hii ya upandaji wa miti iwe endelevu ili kuhakikisha Mindu inapokea maji mengi kutoka katika vyanzo vya maji pamoja na kurudisha Mindu katika ukijani wake unaotakiwa kwani Mindu ya Kijani inawezekana" Amesema Brigedia Jenerali Seif.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Michael Waluse, amesema Manispaa ya Morogoro haipo nyuma ambapo wana wadau ambao wameingia nao mkataba wa kila mwaka kuwapatia miche kwa ajili ya kupanda.
Waluse, amesema Ofisi ya Manispaa ipo wazi inashirikiana na wadau wote wa Mazingira ikiwa na lengo la kuweka Mji safi lakini kutunza vyanzo vya maji visiweze kuharibiwa kutokana na shughuli za kiuchumi zinazofanywa na wananchi.
“ Kwa upande wetu Manispaa ya Morogoro, tunakusudia kupanda miti mingi kwani licha ya kuwa ni agizo la Makamu wa Rais wa Tanzania, Mhe. Mama Samia Suluhu pia ni faida kwa vizazi vijavyo” Amesema Waluse.
Naye, Mkurugenzi wa MORUWASA, Mhandisi Tamim Katakweba, amemshukuru Mkuu wa Wilaya Mhe. Bakari Msulwa pamoja na Bregedia Jenerali ,Seif Hamisi ambaye ni Mkuu wa Kikosi cha Jeshi Mazao Mzinga , kwa kukubali kuhudhuria uzinduzi huo wa Kampeni ya kupanda miti ambapo awamu ya kwanza imepandwa miche ya miti 15000 kati ya miche ya miti ya miche 500000 iliyopangwa kupandwa katika eneo hilo la pembezoni mwa Bwawa la Mindu.
“Leo tumeshuhudia Mkuu wetu wa Wilaya akiongoza Kampeni ya upandaji wa Miti, viongozi na wananchi wamepanda miti ikiwa ni uzinduzi wa Kampeni ya upandaji wa miti katika Vyanzo vya Maji Wilaya ya Morogoro inayosimamia na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Ofisi ya Mkurugenzi Manispaa ya Morogoro , Ofisi ya Bonde la Mto Ruvu, Ofisi ya Idara ya Misitu pamoja na sisi watu wa MORUWASA, niendelee kuchukua nafasi hii kuwaomba wale wakazi wanaofanya shughuli mbalimbali katika ukanda huu wa pembezoni mwa Bwawa watusaidie kuhakikisha kwamba wanakuwa nje ya Mita 60 lakini wajitahidi kuitunza miti hii ambayo ipo katika mashamba yao” Amesema Eng. Tamim.
Katika hatua nyingine, Eng. Tamim, amesema MORUWASA imetenga kiasi cha fedha chenye thamani ya shilingi Bilioni 185 kwa ajili ya maboresho ya huduma za maji Manispaa ya Morogoro ikiwamo kupanua Bwawa la Mindu pamoja na kununua mtambo mpya.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa