MKUU wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Bakari Msulwa, amewataka Watendaji kutatua kero za wananchi kwa wakati badala ya kuendelea kusubiri ziara za viongozi.
Kauli hiyo ameitoa jana , Julai 16, 2020 katika Mkutano wa kusikiliza na kutatua kero za Wananchi uliofanyika kwenye viwanja vya Shule ya Msingi K. Ndege Manispaa ya Morogoro.
Msulwa, alisema ziara hiyo ya Kata kwa Kata imelenga kupunguza kama si kumaliza kabisa kero za Wananchi.
Alisema kuwa kutokana na msimamo huo wa kisheria na kutokana na dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Mhe. Dkt John Pombe Magufuli, katika kutatua kero za wananchi, suala la utatuzi wa kero za wananchi halitakiwi kuendelea kusubiri ziara za viongozi, badala yake, kero hizo zitatuliwe kwenye ngazi zinazohusika na zitatuliwe kwa wakati.
“Tumefika hapa lakini tulichobaini kuwa kero nyingi za Wananchi hazitatuliwi, hii ni kutokana na kutofanyika kwa mikutano kama inavyotakiwa kisheria na Viongozi wa ngazi za chini , Watendaji hakikisheni kero za wananchi wenu mnazitatua kikamilifu, msisubiri mpaka viongozi wa juu washuke chini ,mmepewa mamlaka zote za kusimamia wananchi wenu, mnatakiwa mjiwekee utaratibu wa kuwa karibu zaidi na wananchi kwa kuwafuata katika Kata zao na kufanya mikutano maalum ya kuzungumza na wananchi na kusikiliza kero zao na kuzitatua papo kwa papo” Amesema DC Msulwa.
Aidha, alisema kuwa migogoro mingi na kero nyingi zinasababishwa na kutowajibika kwa baadhi ya watendaji ambao wamepewa dhamana ya kuwaongoza wananchi kwa kuwapatia maendeleo.
Alisema ,suala la kutotatua kero za wananchi katika ngazi ya Serikali za Mitaa ni kinyume na dhamira ya Serikali ya kuwatumikia wananchi wote bila ubaguzi ambalo pia ni kinyume na msimamo wa Ibara ya 146 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Madhumuni ya kuwapo Serikali za Mitaa ni kupeleka madaraka kwa wananchi na vyombo vya Serikali za Mitaa vitakuwa na haki na mamlaka ya kushiriki na kuwashirikisha wananchi katika mpango wa shughuli za utekelezaji wa maendeleo katika Serikali zao na nchi kwa ujumla.”
“Nawasihi viongozi na Wataalamu wa Halmashauri , tembeleeni katika Kata na vijijini na mtatue kero za wananchi huko, lakini hakikisheni mikutano ya mitaa na Vijiji iliyowekwa kwa mujibu wa sheria inafanyika na maazimio yake yanafika kwenye vikao halali vya maamuzi, haiwezekani kuwaacha wananchi wanateseka harafu wewe unajiita mtendaji, kuna kero zinatakiwa kweli Mkuu wa Nchi Mhe. Rais wetu azitatua lakini sio kwa hizi ndogondogo ambazo tunaweza kuzitatua wenyewe tena kwa ngazi za chini kabisa kwa kuwa Serikali yetu imeweka utaratibu wa kiutawala kwa kila ngazi” Ameongeza DC Msulwa.
Naye Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba, amewataka watendaji wa kata, na mitaa kuitisha mikutano ya kisheria ya Mitaa na kata na mitaa na kusoma taarifa za mapato na matumizi ya miradi ya maendeleo katika maeneo yao.
“”Sisi tupo hapa kusikiliza kero za wananachi, tumeona wapo wengine wanashindwa kufika katika Ofisi zetu aidha kwa kukosa muda au nauli, lakini niwaombe Viongozi na Watendaji wa Mitaa na Kata jengeni utamaduni wa kuwatembelea wananchi katika Mitaa yao na kusikiliza kero na changamoto zinazowakabili ikiwa ni pamoja na kuzitafutia ufumbuzi, hizi kero ndogondogo tuzitatue sisi na Mhe. Rais wetu Dkt John Magufuli tumuachie zile kero kubwa na kila mtu akifanya kazi kwa nafasi yake tutafanikiwa na wananchi wetu watapata huduma nzuri zenye viwango zinazoendana na kasi ya Uongozi huu wa Awamu ya tano” Amesema Lukuba.
Katika ziara hiyo, DC Msulwa alipata muda wa kutembelea miradi ya Ujenzi ya Ofisi za Kata ikiwamo Kata ya Chamwino, Mindu pamoja na Uwanja wa Taifa na kuhitimisha na mkutano wa kusikiliza kero ambapo Wananchi wamepata fursa ya kuwasilisha kero na malalamiko yao mbali mbali na Mkuu wa Wilaya kuzitatua papo hapo jambo lililowafurahisha sana Wananchi hao.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa