MKUU wa Wilaya ya Morogoro Mhe.Bakari Msulwa amewataka watu wanaovamia maeneo ya viwanja vya michezo kukomesha tabia hiyo kwani inawanyima fursa vijana kushiriki kwenye michezo.
Kauli hiyo ameitoa leo Septemba 26, 2020 kwenye Viwanja vya Michezo Gymkhana Manispaa ya Morogoro kwenye majadiliano ya kujadili changamoto za Sanaa na Michezo zinazo ikabili Wilaya ya Morogoro.
Akizungumza na Waandishi wa habari, Msulwa, amesema kuwa watu wanaovamia Viwanja vya michezo hawapaswi kuungwa mkono kwani wanawanyima ajira vijana pamoja na maeneo ya kufanyia mazoezi.
Msulwa,amesema kuwa baadhi ya watu wamekuwa wakivamia maeneo ya michezo na kujenga jambo ambalo linakwenda kinyume na matumizi yaliyopangwa na serikali hivyo vijana kushindwa kuendeleza vipaji vyao.
“Watu wenye tabia hii inabidi waiache kwani inadumaza azma ya serikali kuendeleza michezo mbalimbali hapa Wilayani kwetu na nchini kwa ujumla, hasa ikizingatiwa licha ya michezo kuwa ni burudani lakini pia inatoa fursa ya ajira hasa kwa vijana,” Amesema DC msulwa.
Amesema kuwa serikali imekuwa na mipango mbalimbali ya kuendeleza michezo ikiwa ni pamoja na kuwa na viwanja ambavyo vitawawezesha vijana kushiriki michezo hivyo watu wanaovamia na kujenga ni dhahiri wanakwamisha juhudi hizo.
“Tunaomba wadau wa michezo wahamasishe ujengwaji wa viwanja vya michezo, lakini amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri kutoa taarifa za Kata ambazo zina viwanja vya michezo ikiwamo maeneo yaliyovamiwa na watu kuanza makazi ili hatua ziweze kuchukuliwa, lakini niseme kitu kimoja hawa Vijana wanamategemeo makubwa na Serikali yao niwaombe sana Wakurugenzi na Watendaji lazima tujikite katika kuibua vipaji vyao katika nyanja mbalimbali, tukifanya hizi tutatoa ajira na kuwapa uhuru Vijana hawa kuwa na maeoeno ya wazi ya kufanyia mazoezi pamoja na kuendeleza jitihada za serikali kuendeleza michezo hapa nchini” Ameongeza Msulwa.
Katika hatua nyengine, amesema lengo la majadiliano hayo ni
kuwahamasisha vijana kushiriki michezo na sanaa jambo ambalo linatakiwa kupewa uzito wa hali ya juu kwa ajili ya kurudisha hadhi ya Mkoa wa Morogoro katika nyanja ya Michezo.
Mwisho amesema Jumamosoi ijayo ya tarehe 03 Oktoba 2020, watakutana tena na Wanamichezo ili kutoa mrejesho wa yale waliyoyazungumza na kuwekeana mikakati ili kuyafanikisha na kuifanya Morogoro kuwa ya Viwango.
Ikumbukwe kwamba Majadiliano hayo yaliafuatiwa na Mbio za Vijana wa Jogging zilizoanzia katika Viwanja vya Mashujaa majira ya saa 7 asubuhi hadi katika Viwanja vya Ghymkhana ambapo katika mbio za Jogging iliongozwa Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Bakari Msulwa, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro Bi. Rehema Bwasi , Watumishi wa Manispaa ya Morogoro, Jeshi la akiba na Migambo, Vijana wa Jogging mbalimbali, pamoja na Vijana wa Karate Komfuu ambao walishirikia katika majadiliano hayo.
Kwa upande wa mmoja wa wanamichezo, Sylivester Mokiwa, amempongeza Mkuu wa Wilaya ya ubunifu wa kutaka kurudisha hadhi ya Mkoa wa Morogoro katika upande wa michezo.
'"Nichukue shukrani za dhati kumpongeza Mkuu wa Wilaya wetu, kwa kweli tulikuwa hatuna mategemeo kama tutakuja kuwa kitu kimoja lakini sauti zetu zimesikika na tunaona muelekeo mzuri wa Morogoro ya Viwango katika Michezo, niwaombe ndugu zangu tunapoitwa katika majadiliano kama haya tujitokeze kwa wingi, tumempata mtetezi wetu bila shaka sasa heshima ya Morogoro inarejea kwa kasi kubwa""Amesema Mokiwa.
KAULI MBIU : "MOROGORO YA VIWANGO KATIKA MICHEZO INAWEZEKANA"
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa