Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Bakari Msulwa, amezindua Kampeni ijulikayo kwa jina la Pendezesha Mji' Manispaa ya Morogoro.
Kampeni hiyo ya 'pendezesha Mji' imezinduliwa leo Aprili 03/2021 kwenye Kata ya Kilakala kwa kuwashirikisha wadau wa Mazingira , viongozi wa Serikali, Vyama vya siasa , wakuu wa Idara Manispaa ya Morogoro, wafanyabiashara pamoja na Wakazi wa Kata ya Kilakala.
Akiziundua kampeni hiyo , Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Bakari Msulwa, amesema kuwa wamezindua kampeni ya usafi lengo ni kuweka Manispaa ya Morogoro kuwa safi .
DC Msulwa, amesema kuwa Kampeni hii ya usafi itakwenda moja kwa moja ikiwa na malengo ya kumshirikisha kila Mwananchi anayeishi Manispaa ya Morogoro pamoja na Kata zote kuhakikisha anashiriki katika shughuli za usafi.
“ Nilitoa wazo hili la usafi baada ya kuona sasa tunapoelekea sio kuzuri, lakini namshukuru sana Mkurugenzi wetu wa Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba mara baada ya kuzungumza juu ya usafi nimeona hatua za haraka zimeshaanza kuchukuliwa, nawapongeza sana watu wa Mazingira chini ya Mkuu wa idara kwa jitihada mbali mbali za kupambana na suala la usafi , baada ya kutoa maelekezo kwa Mkurugenzi naona wakaanza vikao na hatimaye maelekezo yale waliyashusha kwa Watendaji wote wa Kata kwamba tunaanza Kampeni ya usafi , kubwa zaidi nimefurahishwa sana kuona kampeni hii wananchi wameipokea kwa bashasha sana , nawapongeza sana Watendaji wa kata , watendaji wa Mitaa na Wenyeviti wa Serikali za Mitaa hapa Kilakala kwa uhamasishaji wao ambapo tumeona wananchi, walimu wa shule , wameitikia wito na kutuunga mkono, hatutaishia hapa leo tumezindua na tunatarajia kampeni hii kuwa ya kipekee kwani imezingatia maeneo yote yaliyopo ndani ya Manispaa tuendelee kushikamana kwa pamoja tutafanikiwa na Manispaa yetu itakuwa ya mfano kwa usafi ‘’ Amesema DC Msulwa..
"Kampeni hii tutafika nyumba kwa nyumba, Mtaa kwa mtaa, Kata kwa Kata , na wale ambao watashindwa kuendana na kasi ya usafi wa Mazingira ndani ya Manispaa yetu iwe wananchi au watendaji watachukuliwa hatua kali za kisheria kwa kushindwa kufikia malengo, kikubwa wananchi wafanye usafi na waweke taka sehemu elekezi huku sisi kazi yetu ikiwa ni kupitia na kuzikusanya kuzipeleka dampo , tukishirikiana kwa pamoja changamoto ya usafi katika Manispaa yetu itabaki historia tukumbuke leo tumezindua rasmi kampeni hii ya pendezesha mji Manispaa ya Morogoro lakini sio Morogoro Manispaa pekee bali nataka ujumbe huu ufike Wilaya yote ya Morogoro japo kwa sasa tumeanzia hapa Manispaa, tunataka sasa Viongozi waamke, hususani Watendaji wa Kata tukianza kuzunguka na kufanya Operesheni zetu sisi mtu wa kwanza kushughulika naye ni Mtendaji wa Kata , tunataka Mji wetu uwe safi ukizingatia tunataka kuwa Jiji, hatuwezi kuwa Jiji wakati Mji umezingirwa na mrundikano wa uchafu"" Ameongeza DC Msulwa .
Katika hatua nyengine, DC Msulwa, ameitaka Kampuni ya usafi ya Kajenjere ambayo inahudumia kuzoa taka katika Kata ya Kilakala kuhakikisha inafanya kazi zake kwa spidi kubwa ili taka zinazozalishwa zisiendelee kubaki mitaani.
Mwisho, amesema kuhusu Soko wanatarajia baada ya miezi 2 kufanya uzinduzi wa Soko kwani tayari Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro ameshatenga fedha hizo.
Kwa upande wa Kaimu Mkurugenzi Manispaa ya Morogoro, Enedy Mwanakatwe, amewaagiza Watendaji wa Kata, Mitaa, Maafisa afya pamoja na wananchi waliopo ndani ya Manispaa waibebe kampeni hii na kuichukulia kwa uzito wa hali ya juu sana katika maeneo yao ili yale malengo tarajiwa yaweze kutimia.
"Pia katika uzinduzi huu wa kampeni tutaenda mbali zaidi na kuangalia vyombo vya usafiri ambavyo haiweki vitu vya kuhifadhia taka, kwahiyo tunaomba hata vyombo vya usafiri vianze sasa kuwekewa viwekea taka ili kuweza kulinda na kutunza mji wetu kwani wateja wanaowabeba ni wazalishaji wa taka kwa namna moja au nyingine" Amesema Mwanakatwe.
Kwa upande wa Kaimu Afisa Mazingira Manispaa ya Morogoro, Dausoni Jeremia, amesema kampeni hiyo ya usafi ya pendezesha Mji , italenga katika kusimamia mifereji yote inayozunguka biashara, soko, Viwanda, makazi ya watu, shule pamoja na ofisi ikiwemo ukaguzi wa nyasi ndefu katika maeneo hayo.
‘’Tumezindua rasmi kampeni yetu ya usafi ya pendezesha Mji , lakini hatutaishia hapa tutakuwa na operesheni ya kuangalia wale watu ambao wanaotupa na kumwaga takataka katika mtaa, mitaro wa maji ya mvua, uchochoroni au mahali popote hadharani au katika eneo lolote la wazi bila idhini ya Halmashauri na kuweza kuwachukulia hatua kali za kisheria “ Amesema Jeremia.
Naye Diwani wa Kata ya Kilakala, Mhe. Marco Kanga, ametoa shukrani kwa Mkuu wa Wilaya kwa uzinduzi wa Kampeni huku akiendelea kutoa pongezi sana kwa Uongozi wa Manispaa ya Morogoro kwa kuchagua Kata ya Kilakala kuwa Kata ya kuzindulia Kampeni hiyo ya pendezesha Mji.
Akizungumza Diwani wa kata ya Kilakala amesema tumeipokea vizuri sana kampeni hii, ni jambo zuri na la kiubunifu, nampongeza Mkurugenzi wetu anafanya kazi kubwa sana, idara ya mazingira na vikundi vya usafi, niwaombe wananchi wa kata yangu ya Kilakala tuipokee kwa uzito mkubwa na tushirikiane kikamilifu kwa ajili ya kuweka Kata yetu safi , nawapongeza sana wananchi walioitikia wito na kuja kutuunga mkono na tutashinda vita hii ya usafi na kuifanya Manispaa yetu isonge mbele na tutahakikisha tunashirikiana bega kwa bega ili kuona Kampeni hii inafanikiwa na inazaa matunda'"Amesema Kanga.
Kanga, amesema ni jambo la heshima ambalo Manispaa ya Morogoro imelifanya katika Kata yake huku akimuahidi Mkuu wa Wilaya kuwa maagizo yote aliyoyatoa katika Kampeni hiyo watakwenda kuyafanyia kazi kwa vitendo kwa kushirikiana na Uongozi wa Kata pamoja na Wananchi.
Hata hivyo, Mhe. Kanga, ametoa wito kwa Madiwani wa Manispaa ya Morogoro kuichukulia kampeni hiyo kama suluhisho la usafi ndani ya Manispaa na kuendelea kuhamasisha wananchi waweze kushiriki kikamilifu ili malengo yaliyotarajiwa yaweze kufikiwa.
Katika hatua nyingine, Kanga, amempongeza Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro kwa kuwaahidi kuwapatia kiasi cha Shilingi milioni 30 kwa ajili ya kufufua Soko la Kilakala ambalo mara baada ya kuzinduliwa lilatazalisha ajira kwa Wakazi wa Kilakala na kuongezea mapato Manispaa ya Morogoro.
Hata hivyo,Kanga, amemuomba Mkuu wa Wilaya kuweza kujengewa Kituo kidogo cha Polisi ili kuweza kuimarisha ulinzi na usalama kwa wananchi wa Kata ya Kilakala kwani idadi ya watu ni wengi na ujio wa Soko ndio upo njiani.
Naye mkazi wa Kata ya Kilakala , John Alexander, amesema wao wameipokea kampeni hiyo kwa kishindo kikubwa sana na kuahidi ushirikiano mkubwa dhidi ya Serikali katika kusimamia usafi.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa