Mkuu wa Wilaya ya Morogoro mheshimiwa Rebbeca Nsemwa ametoa pole kwa wananchi wa kata ya Mafisa kwa kupatwa na mafuriko na ugonjwa wa kipindupindu.
Mheshimiwa Nsemwa ameyasema hayo tarehe 14.02.2024 alipotembelea Zahanati ya Sina kujionea maendeleo ya ujenzi wake.
“Ni lazima tujikite kwanza katika suala la usafi. Tujitahidi kuhakikisha maji yote tunayotumia yawe yamechemshwa vizuri kwa sababu ugonjwa wa kipindupindu inasemekana unasababishwa na kula kinyesi, na baadhi ya vyanzo vyetu vya maji vimeathirika sana na mvua nyingi zilizokuwa zikinyesha kwenye maeneo mbalimbali hivi karibuni ” alieza Nsemwa.
Pia, mheshimiwa Nsemwa baada ya kukagua Zahanati hiyo na kujionea vifaa vya kisasa vya kupimia damu (Full Blood Picture), na uwezo wa ini kufanya kazi vikiwepo na havifanyi kazi kutokana na kutokuwepo kwa reagents na friji ya kutunzia reagents, amemuagiza Mkurugenzi wa Manispaa kuhakikisha anapeleka friji ya kutunzia reagents, na kuhakikisha taratibu zinafanyika ili reagents husika zipatikane kwa ajili ya Zahanati hiyo.
Maeneo mengine aliyotembelea ni pamoja na daraja la Mazimbu ambapo ameagiza mto unaopitisha maji kwenye daraja hilo usafishwe ili kuzuia maji yake kuendelea kuchepuka na kuingia kwenye makazi ya wananchi, na mtaa wa Mambi na Sina ambako kuna dampo la maji taka na kuwataka TARURA wajenge barabara kwenyemaeneo hayo ili kupunguza adha ya ukosefu wa barabara zinazopitika wakati wote kwenye maeneo hayo.
Naye Diwani wa kata ya Mafisa mheshimiwa Joel Kisome, akamwomba Mkuu wa Wilaya asaidie kata yake iweze kujengewa mitaro ya kupitisha maji pindi mvua zinaponyesha kwani kukosekana kwa mitaro kunawaweka wananchi wake katika hatari kubwa ya kupata magonjwa ya mlipuko hasa nyakati za mvua.
“Sehemu tuliyopo sio rafiki. Hatuna mitaro, mvua zikinyesha maji kutoka pande zote yanakuja huku. Mto Morogoro nao umehamia huku. Tungepata mitaro tungeshukuru sana” alieleza mheshimiwa Kisome.
Baada ya ziara hiyo, Mkuu wa Wilaya, mheshimiwa Rebecca Nsemwa alifanya mkutano wa hadhara na wananchi wa kata ya Mafisa ambapo alisikiliza kero zao na kuzijibu kwa kushirikiana na Mkurugenzi wa Manispaa na watalamu kutoka TARURA na MORUWASA.
MWISHO
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa