KATIKA kuhakikisha wanafunzi wanasoma kwenye mazingira rafiki na salama Kata ya Chamwino, Diwani wa Kata hiyo Mhe. Abdallah Meya, amekabidhi matofali 500 yenye gharama ya shilingi laki 600,000/= katka katika Shule ya Msingi Kambarage kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa vyumba vya madarasa.
Matofali hayo ameyatoa leo Novemba 17/2022 akiambatana na Uongozi wa CCM Kata ya Chamwino, Uongozi wa Kata wa Serikali , viongozi wa matawi , pamoja na wadau wa maendeleo.
Akizungumza wakati wa kugawa matofali hayo, Mhe. Meya,amesema ameamua kuunga mkono Juhudi za Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan za ujenzi wa madarasa ili wanafunzi wasome katika mazingira rafiki.
Meya ,amesema , wazazi wamekuwa na mwitikio mkubwa wa kuwapeleka watoto wao shule hivyo kufanya idadi ya wanafunzi kuwa kubwa ukilinganisha na vyumba vya madarasa vilivyopo hivyo kupitia matofali hayo 500 aliyoyatoa yatasaidia kupunguza changamoto ya upungufu wa vyumba vya madarasa.
"Nafarijika kuona wanafunzi wakisoma katika mazingira rafiki, niwaombe sana wananchi kuendelea na moyo wa kujitolea katika kufanya kazi za kimaendeleo hali itakayosaidia watoto kusoma katika mazingira mazuri na hatimae kutimiza ndoto zao" Amesema Meya.
Aidha, amewataka wananchi kuwa wazalendo kwa kusaidia shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo kuchimba msingi, kusomba mawe ili kuweza kupunguza gharama zitakazosaidia katika kutekeleza shughuli mbalimbali za kimaendeleo.
Kwa upande wake, Kaimu Katibu wa CCM Kata ya Chamwino, Mwajuma Kibwana, amemshukuru Mhe. Diwani kwa kujitoa kwake huku akiwataka wadau wengine pamoja na wananchi kuchangia maendeleo ya elimu na sio kuwaaachia viongozi na Serikali pekee.
Naye mwakilishi wa Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kambarage, Thecla Kamataita, amempongeza Mhe. Diwani kwa msaada wa matofali 500 ambapo amesema ujenzi wa Madarasa hayo yatakuwa suluhisho la kudumu na itasaidia wanafunzi kusoma vizuri.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa