Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Kebwe Stephen Kebwe amesimamisha vituo vya kuoshea magari vilivyopo katika Halmashauri ya manispaa ya Morogoro kutofanya shughuli hiyo hadi hapo wamiliki wake watakapopokea maelekezo mengine.
Dkt. Kebwe ametoa agizo hilo Disemba 3, mwaka huu mara baada ya kutemebelea vituo kadhaa vya kuoshea magari (Car Wash) vilivyopo katika manispaa hiyo ili kujionea hali halisi na kukuta vituo vingi vinakosa sifa za kufanya kazi hiyo hali iliyosababisha Dkt. Kebwe kutoa agizo hilo.
Miongoni mwa mambo yaliyosababisha vituo hivyo kufungwa ni kukosa sifa ambazo ni pamoja na maeneo kubadilishiwa matumizi, kutokuwa na leseni ya kufanya kazi hiyo, kutililisha maji machafu kwenye vyanzo vya maji, maeneo mengine kutokuwa sehemu sahihi kwa ajili ya kazi hiyo na vingine kukosa sehemu ya kuhifadhia maji taka.
Hata hivyo, Dkt. Kebwe ameagiza kituo cha kuoshea magari cha Oil com kilichopo Nanenane kuendelea na kazi ya kuosha magari kwa kuwa kina mapungufu madogo na kutoa mwezi mmoja kufanya marekebisho yaliyopo ambayo ni kuboresha mifereji ya majitaka kuijengea sakafu ya nzege pamoja na kuweka paa eneo lote la kuoshea magari.
Aidha, Dkt. Kebwe amekisimamisha kufanya kazi kituo cha kuoshea magari cha ‘Double D’ kilichopo kata ya Boma road kwa kuwa kiwanja hicho kipo kwa ajili ya matumizi ya ofisi ya kata na kwamba mabadiliko yoyote yatakayofanyika yapitie kwenye vikao halali vya madiwani wa Halmashauri husika.
Dkt. Kebwe amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Bi. Regina Chonjo kufuatilia maelekezo yote aliyotoa ya kusimamisha vituo hivyo ikiwa ni pamoja na kituo cha kuoshea magari kilichopo kiwanja cha kata ya Boma road na kituo cha kuosha magari kinachomilikiwa na Diwani wa Kata ya Mwembesongo Mhe. Ally Kalungwana ambavyo Dkt. Kebwe ameamuru navyo visimame kufanya kazi hiyo.
“wakati nakwenda kutayarisha maelekezo naombeni msimame kuanzia leo, msimame halafu tutawapa maelekezo nini cha kufanya” alisema Dkt. Kebwe.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa