HALMSHAURI ya Manispaa ya Mpanda yaipongeza Manispaa ya Morogoro kwa usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo ikiwamo mradi wa Soko Kuu la Kisasa, pamoja na Stendi ya mabasi Msamvu.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo, Desemba 18, 2019, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Mpanda , ambaye ndiye kiongozi wa msafara, Mhe. William P. Mbogo, amesema kasi ya miradi ya maendeleo ya Manispaa ya Morogoro imewafurahisha hivyo amelitaka Baraza la Madiwani Manispaa ya Mpanda kuhakikisha wanapo rudi nyumbani waanze kufanya kazi kwa kile walichojifunza.
Amesema kuwa, Manispaa ya Morogoro inahitaji kupongezwa sana kwani wamepiga hatua kubwa huku wakionesha thamani ya fedha katika miradi na wamekuwa mfano wa kuigwa hususani katika miradi hiyo na kuifanya manispaa hiyo kuongeza miradi mingine katika pato lao la ndani.
Pia amefurahishwa zaidi jinsi Manispaa ya Morogoro ilivyoweka vipaumbele hususani katika kuwahamisha wafanyabiashara kwa maridhiano na kuwapa kipaumbele mara baada ya kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa soko kuu.
Aidha, amefurahishwa zaidi kuona Watu wenye uhitaji maalumu wametengewa maeneo yao maalumu, jambo ambalo linalenga kuleta usawa kwa wote na kuendeleza adhima ya Mhe. Rais Dkt John Magufuli ya kuwaendeleza Walemavu , wakina Mama pamoja na Vijana.
"'Niwapongeze viongozi wa Manispaa kazi inaonekana , kwakweli katika miradi yenu kuna vitu vingi tumejifunza, sisi kwetu tuna miradi mingi ikiwamo wa Stendi ya mabasi aidha tumejifunza jinsi ya kuendesha mradi wa soko na tutakwenda kukaa na wafanyabiashara kuona jinsi gani tutawasogeza kwa maridhiano ili kujenga soko manake kujenga soko nje ya mji haitakuwa biashara nzuri kwetu bora tujenge katikati ya mji ili tuweze kupata mapato, pia katika mradi wa stendi ya Msamvu tumeona wakaguzi wa Kimataifa wanavyofanya kazi yao kwakweli inaonesha ni jinsi gani Manispaa yenu mlivyo karibu na Serikali pamoja na Chama Tawala cha CCM" Amesema Mhe. Mbogo.
"Ukiangalia Manispaa yetu ya Mpanda , tunataka kuibua miradi mikubwa lakini tunahitaji kukusanya kodi katika miradi hiyo, hivyo lengo letu kubwa kuja hapa ni kuona namna gani tutapata uzoefu na kujua wenzetu wanatumia aina gani ya ukusanyaji wa mapato na usimamizi wa miradi ili nasisi tuweze kufanya kama wanavyofanya wao " Aliongeza kusema Mhe. Mbogo.
Hata hivyo, amesema watamshauri Mkurugenzi pamoja na Baraza la Madiwani la Halmshauri ya Manispaa ya Mpanda , kuhakikisha mara baada ya kukamilika kwa miradi ya maendeleo waweke uongozi mzuri ambao wataamua katika Baraza lao na utakaokuwa unauwezo wa kukusanya fedha ili Manispaa iweze kuendesha miradi mingine.
Amesema siku zote katika kuhitaji maendeleo lazima ujifunze kwa mwenzako maana rasilimali pesa inakuwa ndogo kuliko idadi ya watu, hivyo wamejifunza jinsi ya kuendesha miradi vizuri, isije tena ikawa wameibua miradi,harafu miradi hiyo ikaleta migogoro na kutokuwa na tija kitu ambacho hakitawasaidia katika kufikia malengo yao ya kukusanya kodi.
Kwa upande wa Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Regina Chonio, ameipongeza Manispaa ya Mpanda kwa kujitolea kuja kujifunza namna ya kuendesha miradi na jinsi ya ukusanyaji wa mapato.
Aidha amesema kujifunza sio dhambi hivyo wataendeleza ushirikiano huo pindi pale watakavyohitajika kufanya hivyo kwa Ustawi wa Maendeleo ya Tanzania na Wananchi kwa Ujumla.
Amesema kuwa kujifunza ni njia ya kupata maendeleo zaidi ,hivyo kwa kupitia mafunzo hayo Manispaa ya Mpanda watanufaika sana na wataimarisha mifumo ya kodi na kuiletea Manispaa yao Mendeleo.
Naye Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba, amesema kuwa , Manispaa ya Morogoro ipo chini kimapato ukilinganisha na Manispaa nyengine za Mjini kama kwenye Majiji makubwa , lakini wanajitahidi sana kufuatilia vyanzo vya mapato , amewahahakishia ushirikiano na kunufaika na lengo la ziara yao yenye kulenga kuwajengea uzoefu na kujua mbinu wanazotumia za ukusanyaji wa mapato.
" Kweli tumewapokea ndugu zetu wa Manispaa ya Mpanda kutoka mkoani Katavi kwa ajili ya kuja kujifunza hapa kwetu, matumaini yangu ni kwamba tangia walivyokuja ni tofauti na sasa baada ya kuondoka, lakini tunachowaambia mafanikio yetu ni kuwa na nidhamu katika matumizi ya fedha za miradi , hivyo tunakusanya fedha nyingi lakini hizi fedha tunazipeleka kwenye miradi ya wananchi na miradi hiyo inaonekana, lakini Manispaa ya Morogoro tumekuwa na miradi mikubwa matarajio yetu baada ya miradi hii kukamilika tutakusanya pesa na tutazielekeza katika kuibua miradi mengine ya maendeleo"Amesema Sheilla.
Aidha, amesema ili kufikia lengo katika ukusanyaji wa kodi ni lazima uheshimu misingi ya matumizi mazuri ya pesa pamoja na kuwekeza katika miradi ya wananchi.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa