Waziri wa Nchi , Ofisi ya Rais , Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Selemani Jaffo ameuagiza Uongozi wa Manispaa ya Morogoro na mkandarasi wa ujenzi wa majengo ya Shule ya Sekondari ya Mji Mpya kukamilisha ujenzi ifikapo Agosti 30, mwaka huu ili wanafunzi waendelee kusoma kwenye madarasa yao.
Waziri Jafo alitoa agizo hilo mjini Morogoro alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa majengo mapya ya shule ya Sekondari Mji Mpya baada ya eneo yalipokuwa awali kupitiwa na njia ya Reli ya Mwendokasi (SGR) .
Alisema , Manispaa hiyo ilichelewa kuanza ujenzi huo tofauti na ilivyo kwa wenzao wa shule ya Sekondari Msoga iliyopo mkoani Pwani ambayo ilipitiwa na njia ya Reli ya SGR.
Waziri Jafo alisema , wenzao mara baada ya kulipwa fidia walianza ujenzi mara moja na tayari umekamilika na wanafunzi wapo shule tangu zilipofunguliwa mapema Julai mwaka huu tofauti na kwa Manispaa ya Morogoro.
“Lakini kwa leo nimeona hapa kazi inaendelea vizuri na ninaagiza kuwa ifikapo Agosti 30, mwaka huu majengo haya yawe yamekamilika na wanafunzi wanakuwa madarasani na mimi nitarudi tena kuona utekelezaji wake “ alisema Jafo.
Waziri Jafo pia alimwagiza Mkurugenzi wa Manispaa hiyo kuhakikisha anaweka mazingira mazuri ya shule hiyo kwa vile ina eneo kubwa tofauti na hapo awali .
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, John Mgalula alisema , walipokea cha fedha Sh bilioni 1.4 za ujenzi mpya wa shule hiyo zikiwa ni fidia baada ya shule iliyokuwa hapo awali kupitiwa na njia ya Reli ya Mwendokasi (SGR) kuvunjwa.
Mgalula alisema , ujenzi wa shule hiyo kwa sasa unaendelea kwa kasi na kwamba watakamilisha kulingana na maagizo yaliyotolewa na Waziri ili wanafunzi waweze kuendelea na masomo hayo .
Kwa upande wake Msimamizi wa Ujenzi wa Shule hiyo kutoka Vikosi vya Ujenzi mkoani Dodoma , Mhandisi Simeon Machibya alimhakikishia Waziri kuwa licha ya kuchelewa kuanza ujenzi huo wataukamilisha ufikapo Agosti 30 ,mwaka huu na kukabidhi kazi.
“ Vifaa vyote vya ujenzi vipo eneo la ujenzi na pia tuna nguvu kazi ya kutosha tumewapata wafanyakazi wa muda wa kusaidia mafundi na wengi ni wanawake ili tutimize lengo lililokusudiwa” alisema Mhandisi Machibya.
Pamoja na hayo alisema ,ujenzi huo ilianza wiki mbili zilizopita kwa kujenga vyumba vya madarasa 20 ,jengo la utawala ,maabara tatu ,nyumba nne za walimu na vyoo matundu 36 kwa matumizi ya wanafunzi na walimu na majengo mengineyo yaliyoanishwa kwenye michoro..
Katika hatua nyingine ,Waziri Jaffo alikagua maenendeleo ya ujenzi wa soko kuu la Morogoro na kuridhishwa na kasi yake na hivyo kuwapongeza wakandarasi wa ujenzi huo pamoja na uongozi wa Manispaa ya Morogoro na kuwataka wakandarasi wengine wazalendo kuiga mfano huo.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa