Waziri wa Nchi , Ofisi ya Rais , Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Suleiman Jafo ameuagiza uongozi wa serikali ya mkoa wa Morogoro kuhamisha fedha kiasi c ha Sh milioni 400 kati ya sh bilioni 1.9 zilizoingizwa katika halmashauri ya wilaya ya Morogoro na kuzipeleka Manispaa ya Morogoro kwa ajili kuanza kuendelea kujenga hospitali ya wilaya ya Manispaa.
Waziri Jafo alitoa agizo hilo hivi karibuni mjini Morogoro kwa mkuu wa mkoa Dk Kebwe Stephen Kebwe , Katibu Tawala wa mkoa pamoja na Mganga mkuu wa mkoa wakati wa ziara yake ya kukagua ujenzi wa soko kuu la Morogoro.
Jafo alisema , kiasi cha Sh milioni 400 zilizoingizwa katika halmashauri ya wilaya ya Morogoro badala ya Manispaa ya Morogoro na kuifanya iwe na jumla ya Sh bilioni 1.9 baada ya awali kuingiziwa sh bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya wilaya.
Hata hivyo alisema , halmashauri hiyo bado haijafanya vizuri katika kusimamia mradi na bado ujenzi wa hospitali yake upo ngazi ya matayarisho na haijaonesha kuzitumia fedha hizo vizuri kwa lengo lililokusudiwa.
“ Nina aagiza Sh milioni 400 walioingiziwa zihamishwe na zielekezwe Manispaa ya Morogoro ambayo haijapewa fedha “ alisema Jafo.
Waziri Jafo alisema, ilifahamika kuwa fedha hizo zimepelekwa Manispaa ya Morogoro , lakini baadaye ikabainika ya kwamba hazikungizwa huko na badala kale zikapelekwa halmashauri ya wilaya ya Morogoro ambako tayari ilipatiwa Sh bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya wilaya.
Kutokana na kuwa na kiasi kikubwa cha fedha na ujenzi wake bado inasuasua alimwagiza mkuu wa mkoa Dk Kebwe , Katibu Tawala wa Mkoa na Mganga mkuu wa mkoa kuzihamisha fedha hizo na kuzipeleka Manispaa kwa ajili ya kujenga hospitali ya wilaya ya Manispaa ili kutoa huduma kwa wananchi.
“ Leo’ Februari 23, 2019 , naagiza hadi jumatano Februari 27 mwaka huu niwe nimepata taarifa ya utekelezaji wake , na nitaipima halmashauri ya wilaya ya Morogoro kwenye utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa hospitali ya wilaya kwa kiasi kilichobakia cha sh bilioni 1.5 sambamba na halmashauri nyingine “ alisema Jafo.
Pamoja na hayo alisema, atapanga kufanya ziara maalumu katika halmashauri hiyo kwa ajili ya kukagua ujenzi wa miradi ya maendeleo ikiwemo ya hospitali hiyo na endapo atakuta bado hawajaanza ama ujenzi wake unasuasua yuko radhi kuhamisha fedha hizo na kuzielekeza maeneo yaliyoonesha kasi kubwa ya ujenzi wa miradi ya kimkakati.
Kwa upande wake Meya Manispaa ya Morogoro , Pascal Kihanga, licha ya kutoa shukrani kwa Serikali ya awamu ya tano kwa kutoa fedha za ujenzi wa miradi ya maendeleo ikiwemo Ujenzi wa vituo vya Afya alisema, Manispaa hiyo haijapewa fedha licha ya wananchi wamejitolea kujenga majengo ya vituo vya afya .
“ Wananachi wetu wamejitokeza kujenga zahanati na vituo vya afya , lakini kama halmashauri bado tumeshindwa kumalizia kwa ukosefu wa fedha za kutosha , tukipata Sh milioni 400 zitatuzaidia kukamilisha majengo haya na kutumiwa na wananchi” alisema Kihanga.
Hivyo alitumia fursa hiyo kumwomba Waziri kuipatia Manispaa hiyo fedha Sh milioni 400 kwa ajili ya kumalizia vituo vya afya ziliojengwa kwa nguvu ya wananchi ikiwemo na hospitali ya wilaya ambayo tayari jengo la utawala lilichajengwa miaka ya nyuma.
Mbali na hayo alimweleza juu changamoto ya jengo la standi Kuu ya mabasi ya Msamvu kuwa tangu agizo la Rais alilolitoa la kukabidhiwa stendi hiyo kwa Manispaa hadi sasa bado hakuna utekelezaji wake na kuwomba waziri asaidie kulishungulikia.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa