Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais , Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, (TAMISEMI) Selemani Jafo ameshangazwa na kusikitishwa na kitendo cha kutotekelezwa kwa agizo la Rais Dk John Magufuli kwa uliokuwa uongozi wa mfuko wa LAPF la kukabidhi uendeshaji wa mradi wa kituo cha mabasi Msamvu kwa Manispaa ya Morogoro.
Waziri Jafo alishangazwa na kauli hiyo baara ya kusikia taarifa kutoka kwa Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro, Pascal Kihanga , kuwa hadi sasa ni zaidi ya miezi minne stendi haijakabidhiwa s wakati alipofanya ziara ya ukaguzi wa ujenzi wa soko jipya la kisasa la Manispaa hiyo hivi karibuni baada ya Serikali kuu kutoa fedha Sh bilioni 17.6 .
“ Nasikia kichefu chefu juu ya jambo hili , Rais aliagiza kuwa stendi ya mabasi ya Msamvu irudi Manispaa ya Morogoro , ni nani mwingine ambaye anayekwamisha utekelezaji huu , wakati akitoa agizo hili nami ( Jaffo) nilikuwepo jukwaani akiwahutubia wananchi wa Morogoro “ alisema Jafo .
Waziri Jafo alisema , Rais aliagiza Stendi ya Mabasi Msamvu irudi Manispaa ya Morogoro kwa kauli yake mbele ya wananchi ( Mei 6, 2018) akiwa jukwaani , hivyo agizo la Rais halina mjadala kinachofuata ni hatua za utekelezaji .
Hata hivyo , Meya wa Manispaa ya Morogoro Kihanga kwa niaba ya uongozi wa halmashauri na serikali ya wilaya na mkoa alimshukuru Rais Dk Magufuli kwa kutoa fedha za ujenzi wa soko la kisasa.
Pia alimshukuru kwa agizo kwa iliyokuwa Menenimenti ya LAPF kukabidhi stendi ya mabasi ya Msamvu kwa Manispaa ili uendeshaji uwe ni wa asilimia 100 , licha ya agizo hilo kushindwa kutekelezwa kwa zaidi ya miezi minne tangu alipofanya ziara na kuzindua stendi hiyo.
Hata hivyo alisema , bado halmashauri ya Manispaa haijakabishiwa Stendi hiyo ingawa yamefanyika majadiliano baina ya pande mbili hizo na kumejitokeza kwa changamoto ya kiwango kikubwa cha fedha Sh bilioni 19 ambacho mfuko unataka ulipwe ili iweze kukabidhi uendeshaji kwa halmashauri wakati haina uwezo huo .
“ Tunakuomba Mheshimiwa Waziri utusaidie jambo hili kwa kuwa Mfuko huu upo chini ya Ofisi yako , tukabidhiwe ili tuweze kuanza kukusanya mapato kwa manufaa ya wananchi wa Manispaa ya Morogoro” alisema Kihanga.
Mfuko wa LAPF kabla ya kuunganishwa mifuko iliyokuwa inahudumia watumishi wa Serikali na kuazishwa mfuko mpya wa PSSSF , iliingia kati yake na Manispaa ya Morogoro kwa kusaini makubaliono kujenga kituo hicho kinachopewa jina la Msamvu Properties Company (T) Limited ambapo umiliki wa hisa ulikuwa ni asilimia 60 kwa Mfuko huo , wakati Manispaa ikiwa na hisa ya asilimia 40.
Hata hivyo Mei 6, mwaka huu (2018) katika hotuba yake ya uzinduzi wa stendi hiyo , Rais Dk John Magufuli alisema kuwa , kutokana na mpango mzuri wa mradi huo na kwa vile serikali imekuwa inatoa fedha za ujenzi wa stendi kama hiyo kwenye halmashauri za wilaya nchini, serikali imeamua kulichukua deni lote lililokuwa ina daiwa na mfuko wa LAPF na kulipwa na serikali.
Katika hotuba hiyo alisema , baada ya kukabidhiwa stendi hiyo na LAPF ,Manispaa hiyo iweke utaratibu wa kuona kwamba kila mfanyabiashara mdogo anapata nafasi ya kufanya biashara katika kufuata utaratibu huo na si kuwabagua ikiwa ni pamoja na kuwa ni kitega uchumi cha kuiingizia mapato yatakayosaidia kuboresha huduma za kijamii.
Kwa mujibu wa taarifa ya uliokuwa uongozi wa wa mfuko huo mbele ya Rais wakati wa uzinduzi huo ilibainisha kuwa , awamu ya kwanza ya ujenzi wa kituo hicho ulikamilika Novemba 2016 kwa gharama ya sh bilioni 12 , pia kulikuwa na uendelevu wa ujenzi wa maduka madogo 80 ambao ulipangwa kuanza juni 2018 kwa gharama ya sh milioni 768.4.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa