WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Jenista Mhagama ameridhishwa na walengwa wa Mpango wa Kuzinusuru Kaya Maskini Manispaa ya Morogoro kwa kuendesha mradi wa funza chuma kwa ajili ya kuzalisha chakula cha mifugo kinachowaongezea kipato na kutatua changamoto ya upatikanaji wa chakula cha mifugo.
Jenista alisema hayo, baada ya kukagua mradi wa kuzalisha funza chuma, unaotekelezwa na walengwa wa TASAF wa kikundi cha Faraja kilichopo mtaa wa Mazimbu Darajani , Kata ya Mazimbu, Manispaa ya Morogoro.
Mpango huo wa Kuzinusuru Kaya Maskini unaoratibiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF)
Alisema kumekuwa na shida ya upatikanaji wa chakula cha mifugo hivyo mradi huo unaotumia teknolojia rahisi kuzalisha funza chuma kwa ajili ya chakula cha mifugo utatatua changamoto ya upatikanaji wa chakula cha mifugo wakiwemo ng’ombe, kuku na Samaki.
“Mmesema hapa kupitia taarifa yenu kuwa, Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimefanya utafiti na kubaini kuwa funza chuma ni chakula kizuri cha mifugo kuliko vyakula vingine ambavyo vimekuwa vikitumika kulisha mifugo na mradi huu ni mzuri na wa kimkakati ambao unapaswa kuendelezwa,”alisema Jenista
Alisema mradi huo utasaidia kuhifadhi mazingira na kutatua changamoto ya uchafu wa mazingira katika masoko kwani badala ya taka kutupwa hovyo ndani ya masoko, zitachukuliwa ili kuzalisha chakula cha mifugo na kuacha masoko yakiwa kwenye hali ya usafi.
“Huu mradi ni suluhisho kubwa la changamoto ya uchumi, uchafu wa mazingira na suala la ajira kwa makundi yote ya akina mama, vijana na wenye ulemavu na walengwa wa TASAF, kwani ni mradi fungamanishi wenye faida nyingi,”alifafanua Jenista
Naye Meya wa Manispaa ya Morogoro,Pascal Kihanga alisema mradi wa funza chuma una faida kubwa katika jamii, kwani utasaidia Manispaa kuwa na mazingira safi na kuboresha maisha ya wananchi kwa kuwaongezea kipato.
“Kutokana na faida ya uwepo wa mradi huu, Manispaa ya Morogoro itawatumia Wahandisi waliopo kuwajengea walengwa wa TASAF na wananchi wengine vizimba vya kufuga funza chuma ili waweze kuzalisha kwa wingi chakula cha mifugo ambacho kitawaongezea kipato chao “ alisema Kihanga.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa Ally Machela alisema katika mwaka wa fedha wa Julai , 2021 hadi Juni , 2022 , Manispaa ilipokea jumla ya Sh milioni 904.2 .
Alisema fedha taslimu zilizolipwa kwa walengwa kwa njia ya mtandao na benki ni Sh milioni 390.9 ambazo zililipwa kwenye namba za simu na akaunti za benki za walengwa moja kwa moja.
“ Manispaa kupitia mpango huu inaendelea kutoa elimu kwa walengwa juu ya matumizi sahihi ya fedha na kuwahimiza kutoa taarifa , kuanzia viongozi wao wa Serikai za mitaa mara anapohama na kuripiwa katika Serikali ya mtaa wanapohamia “ alisema Machela.
Nao baadhi ya wanufaika na mpango huo kwa nyakati tofauti waliishukuru serikali kupitia TASAF kuwawezesha kifedha ambazo wamezitumia kusomesha watoto wao ,kuanzisha miradi midogo ya uzalishaji mali iliyowezesha kuwa na makazi bora .
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa