MBUNGE wa Jimbo la Morogoro Mjini, Abdulaziz Abood, ameliwezesha Jukwaa la Uwezeshaji wanawake Kiuchumi la Manispaa ya Morogoro ( JUWAKIMAMO) vyereheni 25 kwa ajili ya kuanzisha kiwanda cha ushonaji nguo ukiwa ni utekelezaji wa sera ya viwanda kukuza uchumi wa wananchi na taifa .
Mbali na Vyereheni hivyo pia alikabidhi seti moja ya kompyuta , printa , meza na viti kwa Uongozi wa Saccos ya Wanawake Manispaa ya Morogoro (SAWAMAMO) ambapo jumla ya vitu vyote hivyo vimegharimu zaidi ya Sh milioni 20.
Mbunge wa Jimbo alisema kuwa, vyereheni vilivyotolewa kwa Jukwaa hilo ni kwa ajili ya kufungua kiwanda cha ushonaji wa nguzo za aina mbalimbali zikiwemo za wanafunzi, akina mama na za wanaume .
Abood alisema , licha ya kiwanda hicho pia litafunguliwa darasa la kujifunza ufundi kwa watoto wakike waliomaliza elimu ya msingi na sekondari na kushindwa kuendelea ili baadaye waweze kujiajiri wao wenyewe kupitia ujuzi walioupata kwa lengo la kujikwamua kiuchumi.
“ Mradi huu utahusisha pia kuwekwa kwa mashine za kupukucha mahindi na kukamua alizeti … na hii ni kuonesha akina mama wa Manispaa ya Morogoro wanakuwa ni wa mfano Kimkoa kuweza kuwa na kiwanda kitakachowasaidia kujiari na kupata mapato” alisema Abood.
Hata hivyo alisema , mradi huo ni hatua ya utekelezaji wa Ilani ya CCM na pia kuunga mkono juhudi za Rais Dk John Magufuli alizohimiza kuhusu Sera ya Viwanda na akiwa Mbunge wa Jimbo hilo ni wajibu wake kuwa karibu na wananchi kuwasaidia kwa kutoa mchango wake .
“ Kiwanda hiki kitachangia kutoa mchango mkubwa wa kuinua uchumi wa akina mama wa Manispaa ya Morogoro na kutoa ajira kwa wengine “ alisema Abood.
Naye Mwenyekiti wa Jukwaa hilo ,Mary Kachale alimshukuru Mbunge huyo kwa kuwasaidia vyereheni kwa ajili ya kuanzisha kiwanda cha ushonaji nguo ambacho kitasaidia kuwakutanisha wanawake na vijana wakike kujifunza ujuzi wa ushonaji wa nguo ambao utawasaidia katika maisha yao ya kijamii na kiuchumi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Sawamamo Saccos , Beatrice Mogela ,licha ya kumshukuru Mbunge huyo alisema , seti ya Kompyta waliyopatiwa atawasaidia katika utunzaji wa kumbukumbu muhimu na kuondoa gharama za kuchapishaji wa nyaraka za masuala ya kiutawala .
Hata hivyo alisema , Saccos hiyo ina zaidi ya wanachama 900 waliopo kwenye vikundi 13 na ilianzishwa na mtaji wa Sh milioni tano na hadi sasa umefikia Sh milioni 11.8 ambapo utoaji wa mikipo kwa kikundi utaongezeka kutoka Sh milioni mbili hadi milioni 2.3 kuanzia Julai mwaka huu ( 2018).
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa