Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, imetoa taarifa ya ujumla ya watoto 32,093 sawa na 72.5% chini ya umri wa miaka mitano wapata usajili wa vyeti vya kuzaliwa uku Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro akisisitiza wazazi na walezi kuwaandikisha watoto wote ambao hawajaandikishwa kabla ya Machi 15 2020
Taarifa hiyo imetolewa na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro, Mhe. Pascal Kihanga katika Ofisi yake Manispaa ya Morogoro leo Machi 12, 2020.
Akizungumza na Waandishi wa habari, Meya Kihanga, amesema Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro inajumla ya watu 315,866, ambapo Kati ya hao watoto chini ya miaka mitano ni 44,472.
Amesema kuwa, awali zoezi la usajili wa vyeti vya kuzaliwa lilikuwa likitekelezwa na Ofisi za RITA ambao kwa sasa wanaendelea kusajili na kutoa vyeti vya kuzaliwa kuanzia umri wa miaka mitano na kuendelea.
Amesema kuwa tangu mpango wa kusajili vyeti vya kuzaliwa kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano ulipoanza, jumla ya watoto 32,093 (sawa na asilimia 72.5) wamesajiliwa hadi kufikia tarehe 20 Februari, 2020.
Aidha amesema kuwa , kuanzia tarehe 6/12/2019 na kuendelea zoezi la usajili wa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto chini ya miaka 5 linatekelezwa na Halmashauri kupitia Ofisi za kata na vituo vya kutolea huduma za afya vinavyotoa huduma ya baba, mama na mtoto (Kliniki) ambapo vyeti hivyo vinatolewa bila malipo.
Meya Kihanga, amesema vyeti hivyo kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano vina faida kwakuwa ni utambulisho wa awali kisheria utakaomwezesha mtoto kupata haki nyingine kama kuzuia ajira ya watoto na kuwalinda na watu wanaokinzana na sheria, kummsaidia mtoto kuandikishwa shule za Msingi na Sekondari,ni kitambulisho cha msingi ili kupata kitambulisho cha Taifa, Kuwawezesha wanafunzi kujiunga na vyuo na elimu ya juu na kupata mikopo ya elimu ya juu pamoja na kumsaidia kupata hati ya kusafiria ( Passport).
Amesema miongoni mwa vitu muhimu vya kwenda navyo wazazi /walezi katika kituo cha Usajili ni pamoja na nakala ya kadi ya kliniki au tangazo, barua ya mwenyekiti wa Mtaa, Cheti cha ubatizo ambapo aliwataka
Wazazi /Walezi kuhakikisha kwamba ifikapo tarehe 15/03/2020 watoto wote chini ya umri wa miaka mitano wanaoishi Halmashauri ya Manispaa Morogoro kilamtoto awe ameshasajiliwa na kupata cheti cha kuzaliwa.
"Niwaombe wazazi/ walezi wapelekeni watoto wenu wakapate haki yao ya vyeti vya kuzaliwa, kwani zoezi hili la utoaji wa vyeti vinatolewa katika ofisi zote za kata na vituo vyote vinavyotoa huduma ya baba, mama namtoto ( Kliniki), lakini pia cheti hiki cha kuzaliwa kinapatikana bila malipo huku ikibebwa na kauli mbiu ya “ Mtoto anastahili cheti cha kuzaliwa , Mpe haki yake”Amesema Meya Kihanga .
Pia ametoa wito kwa Madiwani pamoja Wenyeviti wa Mitaa wapite katika maeneo yao na endapo kuna watoto hawaja sajiliwa waandikishwe.
Katika hatua nyingine, amezitaja Kata ambazo zimefanya vizuri na zile ambazo hazikufanya vizuri huku akitaja sababu kubwa ya kufanya vibaya kwa baadhi ya Kata ni pamoja na uelewa mdogo wa wananchi, utamaduni wa kusema wenye dhamana wahamasishe zaidi.
Kata ambazo zimefanya vizuri zaidi ya asilimia 100 katika usajili wa watoto chini ya umri wa miaka mitano katika vyeti vya kuzaliwa ni pamoja na Kata ya Kihonda, Mkundi , huku kata zilizofanya vibaya chini ya asilimia 40 ni Kata ya Mbuyuni, Kata ya Magadu, Kata ya Mji Mkuu pamoja na Kata ya Kauzeni.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa