WANANCHI wa mitaa ya Kata ya Kihonda Maghorofani , Manispaa ya Morogoro wameondokana na adha ya kutopata uhakika maji safi na salama baada kujengwa kituo cha kuchota maji ya bomba kupitia ufadhili wa Jumuiya ya Waislamu Waahamadiyya chini ya mradi wake wa Taasisi ya International Association of Ahmadi Architects and Engineers (I.A.A.A.E).
Mkuu wa Chuo cha Ahmadiyya Muslim Jama’at Tanzania, Sheikh Abid Mahmood Bhatti alisema hayo kabla ya kukaribishwa mkuu wa mkoa wa Morogoro, Dk Kebwe Stephen Kebwe , kuzindua mradi wa maji uliojulikana kwa jina la ‘ Water For Life’ katika kituo cha Jumuiya ya Waislamu Waahmadiyya Morogoro na jirani zake .
Alisema , Jumuiya hiyo pamoja na kuwa ni taasisi ya kidini , inayo mipango mbalimbali ya kutoa huduma za kijamii zikiwemo katika sekta ya afya, elimu , umeme na maji.
“ Mradi huu ulianzishwa mwaka jana baada ya kupitishwa na Hadharat Khalifa tul Masih kiongozi mkuu wa Jumuiya ya waislamu waahmadiyya duniani kupitia taasisi ya IAAAE” alisema Bhatti.
Mkuu wa Chuo alisema , jamii ya Kihonda Maghorofani iliyopo karibu na taasisi hiyo wanaweza kuchota maji lita zisizopungua 10,000 kwa siku kwa ajili ya matumizi ya nyumbani .
“ Hapa napenda kuwaomba wananchi kwamba huduma hiii ya kijamii isitumike kwa ajili ya biashara , huduma hii itatolewa bure kwa wakazi wote , bila ubaguzi wa kiitikadi wa kidini na kutolewa kuanzia asubuhi hadi jioni ya kila siku” alisema a Bhatti.
Naye Meneja wa Ahmadiyya Printing Press , Dar es Salaam, Sheikh Basharat Ur Rahman Butt alisema kuwa mradi huo ulianza kwa kuchimbwa kisima cha kina kirefu ambacho ni mita 140 na uwezo wa kuzalisha maji lita 6,000 kwa saa moja .
Alisema kuwa , mradi huo wa Kihonda hadi kukamilika kwake umegharimu kiasi cha Sh milioni 150 pamoja na mwingine mdogo wa Msikiti wa jumuiya hiyo eneo la Masika.
Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Morogoro, Dk Kebwe aliipongeza Jumuiya hiyo kwa kuwajali watu wanyonge kuwasongezea huduma ya mradi wa maji safi na salama ambapo alitumia fursa hiyo kumwagiza Ofisa Mtendaji wa kata hiyo pamoja na Diwani kuhakikisha wanaweka utaratibu mzuri wa ulinzi wa miundombonu ya maji hayo.
Dk Kebwe alisema ,mpango wa serikali hadi kufikia mwaka 2020 huduma ya maji mijini iwe imefikia asilimia 95 ambapo kwa mkoa wa Morogoro huduma hiyo kwa mjini imefikia wastani wa asilimia 71 na kwamba mradi huo ni sehemu ya utelekezaji wa mpango wa serikali wa kufikia lengo hilo.
Nao baadhi ya wakazi wa mtaa wa Kitata , Kata ya Kihonda Maghorofani , Joyce Matemu, Winfrida Laizer pamoja na Aisha Rajabu kwa nyakati tofauti walisema kujengwa kwa kituo cha kuchota maji bure wenye bomba kumetoa unafuu wa upatikanaji maji kila siku .
Walisema mkuwa , kwa muda mrefu wamekuwa wakipata adha ya kusubiri mgao wa kila baada ya siku mbili unaotolewa na Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Manispaa ya Morogoro (MORUWASA).
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa