Kamati ya Huduma za Uchumi, Elimu na afya Manispaa ya Morogoro imeridhia ujenzi wa Kivuko kinachounganisha Mtaa wa Vituli pamoja na Buhomela Kata ya Bigwa .
Kauli hiyo imetolewa leo Aprili 15/2021 katika Ukumbi wa Kingalu Soko Kuu la Morogoro wakati wa majumuisho ya ziara ya Kamati hiyo.
Akizungumza mara baada ya kupitisha maridhiano hayo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Kingo, Mhe. Amin Tunda, amesema kutokana na changamoto waliyoiona ipo haja ya kivuko hicho kuanza kuchukua hatua za ujenzi.
Mhe. Tunda, amesema kuwa, mara baada ya kivuko hicho kukamilika kitasaidia kuondoa adha kwa wananchi ambapo mto huo umepita lakini umekuwa ni njia kubwa ya watu kupita pamoja na kupitisha bidhaa za mazao yao.
"Kamati imeona na imejiridhisha kuwa tuanze utaratibu wa ujenzi mapema, tumeona jinsi eneo hilo linavyutumiwa na watu wengi hususani watu kupita hapo wakiwa na mizigo ya bidhaa kupeleka Soko la Mwanzo mgumu, hii ni adhabu twendeni tukaanze ujenzi japo kunachangamoto ya vivuko vingi lakini hapa tumeona ni jinsi gani wananchi wanavyopta shida wakati wa mvua zinaponyesha huku shughuli zao za uchumi zikisimama" Amesema Tunda.
Kwa upande wa Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba, amesema kuwa changamoto zipo nyingi za vivuko pamoja na barabara , hivyo japo vyengine havipo katika bajeti lakini wataangalia ni kwa namna gani wanatatua changamoto hizo zinazowakabili wananchi.
Lukuba, katika kutoa majibu hayo, amemuagiza Mchumi wa Manispaa ya Morogoro pamoja na Mhandisi wa Manispaa kuangalia njia gani ambayo wanaweza kuanza nayo ili kuchukua hatua za awali.
Naye Mjumbe wa Kamati hiyo ambaye pia ni Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro, Mhe. Pascal Kihanga, amesema ni bora ujenzi ukaanza kwani kivuko hicho kimekuwa kikitumiwa na wakazi wengi ambao wametenganishwa na mto.
Kihanga, amesema kuwa ujenzi wa vivuko pia uendane na ujenzi wa ukarabati wa barabara kwani asilimia kubwa ya Kata za pembezoni barabara zake hafifu na hazipitiki jambo ambalo linakwamisha shughuli za maendeleo kufanyika.
Kwa upande wa Mhe. Thomas Butabile, Diwani wa Kata ya Mafiga, amesema ni bora eneno hilo likaangaliwa kwa jicho la tatu kwani wakazi wengi wa Bigwa wanaotumia eneo hilo linalohitaji kivuko ni wafanyabiashara.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa