Kamati ya kudumu ya bunge ya katiba na sheria imetembelea na kukagua vikundi vinavyopewa mikopo na Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro ikiwa ni agizo la Serikali la Kutenga asilimia 10 ya mapato yake kwaajili ya kutoa mikopo kwa vijana,wanawawake na watu wenye ulemavu.
Kamati hiyo ya Bunge ilifanya ziara Oktoba 26,na kukutana na vijana wa kikundi cha Mazimbu Agro kinachojishughulisha na ukoboaji wa mpunga ambao walipewa mkopo wa Tsh Mil 6, na kikundi cha Facaweso(Faraja Capentry welding and social service) kinachojishughulisha na uchongaji wa fenicha za majumbani ambao wamepewa mkopo wa Tsh mil 2.
Akitoa taarifa mbele ya Kamati hiyo Mkurugenzi wa Manispaa Sheila Lukuba ameieleza kamati hiyo ya bunge kuwa Halmashauri imekuwa ikitenga asilimia kumi ya mapato ya ndani kwa ajili ya kutoa mikopo kwa vikundi vya vijana,wanawake na watu wenye ulemavu huku akibainisha baadhi ya changamoto katika kuvisimamia vikundi hivyo.
Nao vijana waliopatiwa mikopo na Manispaa ya Morogoro wamelezea wamenufaika na mikopo hiyo na kwamba imewawezesha kuzalisha ajira kutoka ishirini na tano hadi sitini na nane kila mwaka na kutoa fursa za ajira kwa vijana hao.
Wakizungumza wakati wa ziara ya kamati ya kudumu ya bunge ya katiba na sheria ya kugagua miradi hiyo vijana hao Bw James Luanda na Alexender Nikonia wamesema miradi hiyo imewawezesha vijana kujiajiri wenyewe kupitia miradi wanayoianzisha na kujiongezea kipato sambamba na kila mwanavikundi kuanzisha miradi binafsi huku wakibainisha changamoto zinazowakabili ikiwemo mikopo kutokidhi mahitaji ya mitaji pamoja na kukosa maeneo ya kuendesha biashara zao.
Katika ziara hiyo ikiongozwa na Makamu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge,katiba na sheria Mheshimiwa,Najma Giga amesema kuwa mikopo hiyo imelenga kuwasaidia vijana kujiajiri na kujikwamua kiuchumi huku Naibu waziri wa kazi,ajira,vijana na watu wenye ulemavu Anthony Mavunde akizitaka Halmashauri zote nchini kutenga asilimia kumi ya mapato ya ndani kwa ajili ya mikopo kwa vijana na akina mama.
Halmashauri zinatakiwa kutenga asilimia nne ya mapato yake kwa vijana na asilimia nne nyingine kwa wanawake huku asilimia mbili ikilenga watu wenye ulemavu.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa