KAMATI ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi CCM Wilaya ya Morogoro, imeipongeza Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kufuatia kujenga kwa ubora na kasi kubwa jengo la Ofisi ya Uthibiti Ubora wa Shule Manispaa ya Morogoro.
Hayo yamezungumza na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Morogoro, Ndg. Fikiri Juma , wakati wa ziara ya kutembelea miradi yote ya maendeleo inayoendelea kutekelezwa na Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Akizungumza na Waandishi wa Habari , amesema kasi na ubora wa Ujenzi unaonesha dhahiri Manispaa imekimbizana na inastahili pongezi ya hali ya juu kwani licha ya ubora lakini imeonesha ni jinsi gani imezingatia thamani ya pesa iliyotumika.
Aidha, amesema kuwa kama viwango hivyo , vilivyotumika katika mradi huo wa Ofisi ya Uthibiti Ubora wa Shule vikitumika katika miradi mingine Manispaa ya Morogoro itapiga hatua na kutoa huduma bora kwa Wananchi.
Amesema kuwa Ujenzi huo umeonesha thamani ya pesa iliyotumika , hivyo ameiagiza Manispaa ya Morogoro kuhakikisha inasimamia vizuri na miradi mingine inayoendelea kutekelezwa na ile ambayo itatekelezwa.
Pia amemuomba Mthibiti wa Ubora wa Shule Manispaa ya Morogoro kuhakikisha katika majukumu yao wanawashirikisha Manispaa , Maafisa Elimu, Waalimu wakuu wa Shule, pamoja na Bodi za Shule ili kuangalia ni kwa namna gani wanaweza kufanya kazi pamoja na kuleta maendeleo chanya katika suala zima la taaluma Shuleni.
" Nafahamu kwamba mpo chini ya Wizara ya elimu , shirikianeni na Manispaa , lakini niwaombe taaluma yoyote haiwezi kupanda kama Mtoto hajapata chakula vizuri , licha ya kufanya kazi za uthibiti ubora lakini suala la lishe kwa wanafunzi ni jambo la kulipa kipaumbele sana, niwaombe na kuwashauri katika vikao vyenu hakikisheni wajumbe wa bodi wanakwenda kushirikiana na Madiwani ambao wana ushawishi mkubwa wa kuongea na Wazazi ili waweze kuchangia chakula shuleni na watoto wafanye vizuri katika masomo yao" Amesema Fikiri
Amesema kuwa Shule nyingi hapa nchini zimetumia sana fedha katika ujenzi Mhe. Rais Dkt John Magufuli amejitahidi kuwekeza katika mpango wa Elimu bure bila malipo, hivyo ni wajibu wa kuhakikisha pamoja na ubora wa shule lakini matokeo yaonekane katika viwango vya ufaulu.
Hata hivyo, Mwenyekiti Fikiri amempongeza Mhandisi wa Manispaa ya Morogoro, Eng. Juma Gwisu kwa kazi nzuri anazozifanya katika kusimamia ubora wa miradi.
Kwa upande wa Mthibiti wa Uthibiti Ubora wa Shule Manispaa ya Morogoro, Bi. Victoria Michael Bengesi, amesema kuwa Manispaa ya Morogoro ni miongoni mwa Halmashuri 100 nchini, zilizo katika mpango wa Serikali wa kujengewa Ofisi za Uthibiti Ubora wa Shule Wilaya.
Bi Victoria amesema kuwa mradi huo ulianza kutekelezwa tarehe 1, Julai, 2019 kwa kipindi cha miezi mitatu ya utekelzaji hivyo kuchelewa kwake kumechangiwa na baadhi ya changamoto kama vile kutokuwepo kwa maji eneo la ujenzi, kuchelewa kwa vifaa kama vile Saruji na mabati kutoka kwa msambazaji hasa wa Viwanda kwa takribani wiki mbili na kuchelewa kupatikana kwa matofali yanayofaa kutoka kwa msambazaji aliyeteuliwa.
Aidha amesema mradi huo umegharimu jumla ya Shilingi Milioni 152 ambapo pesa hizo zimejumusiha gharama ya ujenzi pamoja na ununuzi wa samani na vifaa.
"Utekelezaji wa mradi huu umekamilika kwa asilimia 100, hivyo kwa sasa shughuli zinazoendelea ni pamoja na ufungaji wa milango, upigaji wa rangi awamu ya mwisho, uwekaji wa marumaru eneo la vyoo vya ndani pamoja na ufungaji wa mfumo wa umeme" Amesema Bi. Victoria
Katika hatua nyengine, amesema licha ya shughuli hizo kuendelea , zipo shughuli nyingine za ziada ambazo zimeongezeka kutokana na uhitaji na mazingira halisi ya ofisi ilipo.
Miongoni mwa shughuli hizo ni pamoja na Uwekaji wa uzio kwa ajili ya usalama wa Ofisi, Ujenzi wa kibanda cha mlinzi, Ujenzi wa Choo cha nje chenye matundu mawili na Ujenzi wa Karavati ili kuwezesha uingiaji na utokaji katika eneo la Ofisi kwa urahisi.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa