Mwenyekiti wa Kamati ya ulinzi na usalama Manispaa ya Morogoro ambaye pia ni mkuu wa wilaya ya Morogoro Mhe. Regina Chonjo ameagiza kukamatwa kwa mkandarasi wa kampuni ya ujenzi ya Fast kutokana na kushindwa kufuata masharti ya mkataba wake ya kukamilisha ujenzi wa mradi wa stendi ya dalala kaloleni.
Akiongea na waandishi wa habari baada ya kamati hiyo kufanya ziara ya kutembelea miradi mbalimbali Manispaa ya Morogoro Mhe. Chonjo amemuagiza kaimu Kamanda wa polisi Wilaya(OCD), na TAKUKURU kushirikiana kuharakisha zoezi la kukamatwa kwa mkandarasi huyo kabla ya jumamosi tarehe 18 ili aeleze sababu za msingi za kushindwa kukamilisha mradi huo na kurejesha fedha alizopewa kama malipo ya awali kiasi cha Tsh 108,714,375.00 kwa kuwa kazi iliyofanyika eneo la mradi haizidi ata milioni tano.
Aidha ameagiza ufuatiliaji ufanyike katika benki iliyomuwekea dhamana mkandarasi huyo ya China Commercial na kuona kama benki hiyo ina tawi ndani ya Tanzania.
"kuanzia leo hakuna benki ya nje ya nchi itakayomwekea dhamana mkandarasi yoyote anayefanya kazi ndani ya Manispaa ya Morogoro,tafuteni benki za hapa nchini ambazo zina matawi katika mikoa yote ili iwe rahisi kuzifatilia pindi wakandarasi wanaposumbua"Alisema Mhe.Chonjo.
Naye Mstahiki meya wa manispaa ya morogoro Mhe. Pascal Kihanga ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya Fedha na Uongozi Manispaa amesema kama kamati wameamua kuvunja mkataba kutokana na mkandarasi huyo kushindwa kufanya kazi kwa mda aliopangiwa kwa mujibu wa mkataba ili kunusuru fedha za mkopo wa benki ya dunia chini ya mpango wa uboreshaji miji (ULGSP) zilizotolewa kwa ajili ya ujenzi wa stendi hiyo.
Kwa upande wake msimamizi wa mradi huo meneja wa TARURA w Manispaa ya Morogoro Mhandisi James Mnene amesema inavoonekana mkandarasi huyo ameshindwa kufanya kazi hiyo kwani hadi sasa amefanya kazi kwa asilimia 15 ikiwa ni nje ya mkataba wake unavosema na hadi sasa alitakiwa kuwa amefanya kazi kwa asilimia 96 na alitakiwa kukabidhi kazi hiyo ifikapo Januari 19,2020.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa