Katibu Mkuu OR-TAMISEMI Mhandisi Joseph Nyamhanga amemwagiza mkandarasi anayesimamia ujenzi wa shule ya sekondari Mjimpya kukamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa ifikapo mwezi Agosti 2019 ili wanafunzi waliohamishiwa shule ya Sekondari Tushikamane waweze kurudi shuleni hapo na kuendelea na masomo.
Mhandisi Nyamhanga ametoa agizo hilo leo alipofanya ziara ya kutembelea na kujionea maendeleo ya ujenzi wa shule hiyo,ambayo awali shule iliyokuwepo imevunjwa ili kupisha ujenzi wa reli ya kisasa.
"Naagiza shule hii kukamilika ndani ya mwezi Agosti,Serikali imeleta fedha kiasi cha Tsh 1,430,000,000.00 kwaajili ya ujenzi,hivyo zifanye kazi iliyoombewa na kwa viwango vinavyotakiwa "alisema Mhandisi Nyamhanga.
Aidha Mhandisi Nyamhanga alihoji kuhusu uchelewaji wa mkandarasi kuanza kazi wakati Serikali ilituma fedha toka mwezi April 2019,na kujibiwa na Mkurugenzi wa Manispaa John Mgalula kuwa kilichochelewesha ni taratibu za manunuzi ili kumpata mkandarasi atakayefanya kazi hiyo.
Aidha Mkurugenzi Mgalula alieleza kuwa baada ya taratibu kukamilika ofisi iliipata kampuni ya vikosi vya ujenzi kutoka Wizara ya Ujenzi(Corporation Sole works Superintendent )ya Dodoma na kwa mujibu wa mkataba anatakiwa kufanya kazi kwa mda wa miezi minne na atatakiwa kukabidhi kazi ifikapo tarehe 25/10/2019,na hadi sasa kampuni imeshalipwa asilimia 50 sawa na Tsh 715,000,000.00 kama malipo ya awali.
Mgalula alieleza kuwa hadi sasa jumla ya misingi ya madarasa 20,maktaba moja,vyumba vya kompyuta vitatu,vyoo,nyumba za walimu tayari ujenzi wake umeshafanyika na kwasasa mkandarasi anajiandaa kuanza kupandisha kuta za majengo hayo.
Pia Mhandisi Nyamhanga alitembelea shule ya Sekondari Tushikamane ambayo ndiyo imehamishiwa wanafunzi kutoka shule ya sekondari Mjimpya na kuagiza uongozi wa Halmashauri kujenga choo kingine haraka ili kuendana na uhalisia wa wanafunzi waliopo shuleni hapo.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa