Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Prof. Riziki Shemdoe, amefanya ziara ya kutembelea katika Mabweni yaliyoungua na moto shule za Sekondari mbili ikiwemo shule ya Wasichana ya Kiislamu ya AT-TAAUN na Shule ya Sekondari Charlotte zilizopo Manispaa ya Morogoro.
Ziara hiyo imefanyika leo, Julai 11/ 2020 akiambatana na Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mhe. Albert Msando, Kamati ya ulinzi na usalama , Kamanda wa Jeshi la ZimaMoto na Uokoaji Mkoa wa Morogoro , Goodluck Zelote, pamoja na Uongozi wa Manispaa ya Morogoro ukiongozwa na Kaimu Mkurugenzi Pili Kitwana.
Katika ziara hiyo, Prof. Shemdoe, amesikitishwa na uharibifu wa moto ulioteketeza mali za wanafunzi huku akiwataka walimu, wanafunzi pamoja na Uongozi wa shule kuwa na subra katika kipindi hiki kifupi cha mpito.
Prof. Shemdoe, amewaomba Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Jeshi la zima moto na uokoaji Mkoa wa Morogoro washirikiane vyema katika kufanya kutathmini madhara yaliyojitokeza kutokana na moto huo ili Serikali iweze kuwa na taarifa kamili na kujua nini kinaweza kufanyika .
Mwisho, Prof. Shemdoe, amewataka wasimamizi wa Shule kuhakikisha wanafanya maboresho ya mifumo ya umeme mara kwa mara ili kuweza kuzuia majanga kama hayo kutokea.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Albert Msando kwa niaba ya mkuu wa Mkoa wa Morogoro , amemshukuru Prof. Shemdoe kwa ziara yake na kuwatia moyo waalimu, wanafunzi pamoja na Uongozi wa Serikali.
DC Msando, amesema kuwa tayari wao kama Viongozi wa Serikali mara baada ya kupata taarifa ya kuungua kwa mabweni , wamechukua hatua ikiwemo ya kuhakikisha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji linafika eneo husika na kufanikisha kuuzima moto huo katika shule hizo mbili.
"Tumeona madhara yaliyotokea katika mabweni ya shule zetu, Jeshi la zimamoto limefanya kazi yake vizuri, nawapa pole sana, lakini kikubwa niwasisitize wasimamizi wa shule waendelee kuchukua tahadhari zote muhimu ili majanga kama haya yasijitokeze tena, naomba sana Uongozi wa Shule husika wawe na subra katika kipindi hiki cha uchunguzi naamini tukishajua chanzo ni nini , basi tutawapa taarifa sahihi juu ya nini kinapaswa kufanyika" Amesema DC Msando.
Kwa upande wa Mkuu wa Shule ya Sekondari Charlotte , Sister Agness Wilson, amemshukuru Katibu wa TAMISEMI, Uongozi wa Mkoa , Wilaya na Manispaa na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa kuwa karibu sana na matatizo yaliyowakumba huku akisema ujio wa viongozi hao umewatia moyo wa kuendelea kufanya kazi .
" Tunawapongeza sana Viongozi wetu , ujio wao umetupa nguvu na matumaini, ukiangalia hapa madhara makubwa ni kuungua kwa vitu , moto huu ulitokea Julai 10, majira ya saa 3 asubuhi lakini tunamshukuru Mungu aliweza kutuepusha na janga hilo, hakuna aliyefariki wala kujeruhiwa, zaidi tu ni kuungua kwa bweni la kidato cha kwanza wasichana ambapo tukio hilo linatokea wao walikuwa madarasani, tukawahamisha wote ambao wamekutwa na majanga kuwaweka katika mabweni ya wanafunzi wa Pre- Form 1, lakini sasa tunaendelea vizuri na wanafunzi wanasoma kama kawaida licha ya matatizo hayo" Amesema Sister Agness.
Shule ambazo mabweni yao yamepatwa kuunguliwa kwa moto ni pamoja na shule ya Kiislamu ya Wasichana ya AT-TAAUN iliyopo Kata ya Mji Mpya ambapo bweni la ghorofa ya juu yenye vyumba 6 vya madarasa vinavyobeba jumla ya wanafunzi 120, pamoja na Shule ya Sekondari Charlotte iliyopo Kata ya Tungi ambayo imeungua bweni moja la wanafunzi wa kidato cha kwanza upande wa wasichana.
Mpaka sasa jeshi la Polisi Wilaya ya Morogoro kwa kushirikiana na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Morogoro wapo katika hatua za kufanya tathmini juu ya madhara yaliyosababishwa na janga hilo kisha baada ya kupata taarifa itawasilisha katika mamlaka ya juu ili kuona nini kinapaswa kufanyika.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa