MKUU wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amesema kazi yake ya kwanza kama Mkuu wa Mkoa huo ni kuhakikisha kuwa kuna Amani na Utulivu ndani ya Mkoa kwa ajili ya wana morogoro pamoja na wawekezaji wanaotamani kuja kuwekeza ndani ya Mkoa huo.
Mhe. Kigoma Malima amesema hayo Mei 26, 2023 wakati wa kikao cha kujitambulisha kwa Wajumbe wa Sekretarieti ya Mkoa huo kilichofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro ikiwa ni mara yake ya kwanza kufanya kikao na wajumbe hao tangu alipoteuliwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan wiki moja iliyopita kushika nafasi hiyo.
Amesema, jukumu lake la kwanza kama Mkuu wa Mkoa ni kulinda Amani na Utulivu viwepo hivyo wananchi kuendelea kufanya kazi zao za uzalishaji mali kwa Amani na utulivu lakini pia Amani hiyo itawezesha wawekezaji kuvutiwa kuja kuwekeza ndani ya Mkoa wa Morogoro
“Kwa hiyo, kazi yangu ya kwanza ni kuhakikisha kwamba Morogoro ina misingi ya AMANI na UTULIVU inayoongoza wananchi kufanya kazi zao ” amebainisha Mhe. Adam Malima.
Aidha, amesema jukumu lake la pili ni kusimamia maendeleo ya wananchi wa Morogoro na ya Serikali kwa ujumla kwa kuangalia na kushauri utekelezaji wa miradi hiyo ya Serikali inayotekelezwa ndani ya Mkoa huo.
Hata hivyo, amesema ili kutekeleza majukumu hayo makubwa ushirikiano unahitajika, kwa kuwa peke yake hawezi kukamilisha azma hizo za Mkoa na Serikali ya awamu ya sita, isipokuwa ni kwa kufanya kazi kama timu.
Akisisitiza suala la ushirikiano amesema kwenye suala la Amani, Wajumbe wa kamati ya Ulinzi na Usalama watatakiwa kumpa ushirikiano wa kutosha ili kuendelea kudumisha Amani ya Mkoa na kwa upande wa usimamiaji wa miradi ya maendeleo Wajumbe wa Sekretarieti ya Mkoa wanatakiwa kuwajibika na kutoa ushirikiano huo kwake.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa huo Dkt. Mussa Ali Mussa amewataka wajumbe wa Sekretarieti ya Mkoa huo kubadilika na kufanya kazi kulingana na wakati na mazingira yaliyopo badala ya kuendelea kufanya kazi kwa mazoea.
Aidha, amewataka Wajumbe hao kuwa na desturi ya kuwasiliana baina ya idara moja na idara nyingine katika utekelezaji wa majukumu yao jambo ambalo amesema bado ni changamoto katika taasisi hiyo.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa