Wakuu wa Divisheni na Vitengo wa Manispaa ya Morogoro kwa kushirikiana na walengwa wa TASAF wa Kata za Sultan na Mji Mkuu, leo, tarehe 08.12.2023, wamepanda miti 85 kwenye eneo la mto Kikundi, ikiwa ni mojawapo ya shughuli ambazo Manispaa ya Morogoro inazifanya kuelekea katika maadhimisho ya miaka 62 ya Uhuru wa Tanzania Bara.
Kwa mujibu wa Afisa Mazingira wa Manispaa ya Morogoro, ndugu Dauson Jeremiah, miti hiyo iliyopandwa leo, imekabidhiwa kwa walengwa wa TASAF wa Kata za Sultan na Mji Mkuu ili waitunze mpaka itakapokua lakini pia kwa kuwa zana ya mazingira ni shirikishi, ndugu Dauson amewataka wananchi kuhakikisha wanailinda miti iliyopandwa na kuhakikisha inakua.
Ndugu Jeremiah amesema, kitengo cha mazingira cha Manispaa ya Morogoro kilianzisha mashuleni Kampeni ya Soma na Mti ambapo kila mwanafunzi anatakiwa kupanda mti mmoja na kuhakikisha anaulinda na kuuhudumia hadi utakapokuwa mkubwa.
“Mbali na Kampeni hiyo ya Soma na Mti, hivi sasa ili mtu apate kibali cha Manispaa cha ujenzi ni lazima awe amepanda miti mitatu katika eneo analotazamia kufanya ujenzi ndipo aweze kupatiwa kibali hicho. Vilevile, hivi karibuni tumeanza Kampeni nyingine inayotaka kila nyumba ipande miti mitatu ya kivuli na tayari mpaka sasa tunayo jumla ya miti 20,000 ambayo tumeshaanza kuigawa bure kwa wananchi ili waweze kuipanda majumbani mwao” alieleza Jeremiah.
Kwa upande wake mtendaji wa mtaa wa Ukwele na Kota, Bi. Fatuma Said amesema yeye kama msimamizi wa shughuli za Manispaa ndani ya mtaa wake atahakikisha miti yote iliyopandwa inalindwa na kutunzwa vyema kwa ajili ya kuendelea kuhifadhi mazingira ya eneo hilo.
"Nitaendelea kutoa elimu kuhusu utunzaji wa miti hii kwa wafanyabiashara ambao muda mwingi hasa Jumamosi huwa wanafanya biashara zao karibu na mto huu wa Kikundi. Vilevile, nitasimamia vyema walengwa wa TASAF wa eneo langu waliokabidhiwa miti hii ili kuhakikisha wanaitunza" alisema Bi.Fatuma.
Aidha, kabla ya zoezi la upandaji miti, wakuu wa Divisheni na Vitengo pamoja na watendaji wa Kata wa Manispaa ya Morogoro walifanya usafi wa mazingira ya Soko Kuu la Kingalu.
MWISHO
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa