KAMATI ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) , imeipongeza Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kwa usimamizi mzuri wa ujenzi wa Soko kuu la kisasa.
Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Vedastus Ngombale, ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Kilwa Kaskazini, baada ya kamati hiyo kufanya ziara katika mradi wa Soko Kuu la Kisasa na kupitia ripoti ya mradi wa soko hilo.
Akizungumza na Waandishi wa Habari , Januari 10,2020, Mhe. Vedastus, amesema kasi ya mradi huo imewafurahisha hivyo ameitaka Manispaa kuhakikisha sehemu iliyobakia ya ujenzi inakamilika kwa wakati uliopangwa.
Amesema kuwa, Manispaa ya Morogoro inahitaji kupongezwa sana kwani kabla ya pesa za ruzuku ya Serikali katika Miradi Mikakati tayari Halmashauri ya Manispaa ilishaanza kutafuta pesa kwaajili ya ujenzi , hizi ni juhudi kubwa sana , hatua iliyofikiwa ya mradi imeonesha thamani ya pesa iliyotumika japo kuna mapungufu madogo madogo lakini naimani watakaa na kuyaweka sawa .
Amemshauri Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro pamoja Mkurugenzi wa Manispaa kuhakikisha kwamba mara baada ya kukamilika kwa mradi wa Soko kuu la kisasa waweke uongozi mzuri ambao wataamua katika Baraza la Madiwani na utakaokuwa unauwezo wa kukusanya fedha ili Manispaa iweze kuendesha miradi mingine.
"'Niwapongeze viongozi wa Manispaa kazi inaonekana fedha kidogo kazi kubwa , kwakweli mradi huu tutautangaza kwa Mhe. Rais Dkt . John Magufuli kuonesha jinsi gani mlivyokuwa makini katika matumizi ya fedha, pia niwaombe mjifunze katika miradi ya wenzenu ili muweze kuendesha soko vizuri, isije tena mkawa mmeleta mradi harafu mradi huo ukaleta migogoro na kutokuwa na tija kitu ambacho hakitawasaidia katika kufikia malengo ya kukusanya kodi".Alisema Mhe.Vedastus
Katika hatua nyingine, ameutaka Uongozi wa Halmashauri kuhakikisha wanaweka viwango vya bei rafiki na nafuu kwa Wafanyabiashara ili waweze kufanya biashara katika kupata vipato vyao na Halmashauri kuingiza mapato.
Amesema Mhe. Rais Dkt John Magufuli uwa hana utani katika fedha anazozitoa katika miradi , hivyo anataka kuona pesa anazozitoa zinatumika kwa miradi iliyokusudiwa na kuleta tija kwa Wananchi na kuona watu wa chini wananufaika na miradi hiyo.
Kwa upande wa Makamu Mwenyekiti wa LAAC na Mbunge wa Jimbo la Nanyamba Mtwara,Mhe. Abdallah Chikota , ameshauri Uongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, kujiandaa vyema kupokea mradi huo wa soko.
Amesema kuwa, mradi huo ni mkubwa lazima wahakikishe wanaunda timu ndogo ya Wataalamu ili mradi usiishie kati kwa ajili ya kuendesha Soko hilo au kuajiri hata kwa muda wataalamu kutoka nje badala ya kumtegemea Afisa Biashara jambo ambalo watashindwa kufikia malengo.
Pia amewashauri Mwanasheria pamoja na watu wa uchumi Manispaa waangalie miongozo ya fedha kutoka katika Wizara ya fedha ili kuona gharama na makusanyo wakati wanakwenda kuandaa mikataba ya uendeshaji wa Soko hilo.
Pia katika upande wa maegesho ya magari ameshauri wasiangalie makusanyo waangalie gharama za makusanyo kwani mradi huo ni wawananchi wakifanya bei kubwa watawakimbiza wateja na watakosa watu wa kuwaingizia mapato.
Hata hivyo, Mbunge wa Viti maalumu Mtwara Mjini, Mhe. Tunza Malapo, ameitaka Manispaa kuangalia upya suala la tozo za maegeshho kutoka Shilingi 3000/= kwani bei hiyo ni kubwa na ukizingatia mradi huo ni wa wananchi.
Amesema athari ya kuwa na bei kubwa kutafanya iwakimbize wateja na kutafuta mahala pengine kwa ajili ya kupata huduma lakini manispaa itakosa watu na malengo waliyojiwekea ya makusanyo hayatakwenda kama wanavyotarajia.
Naye, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba, ameupongeza Uongozi wa LAAC kwa kutembelea mradi wa Soko kuu la kisasa na kujua maendeleo yake.
"Katika mradi huu katika kuupokea tumeshirikiana na wadau na wale wafanya biashara ambao walikuwa wakifanya biashara katika Soko la zamani tuliwaondoa na kuwapeleka soko la manzese na mitaani lakini kwa mikataba ili tutakapo maliza soko letu vipaumbele vya kwanza vitakuwa ni wao na mambo mengine baraza la madiwani tutakaa na kuona ni utaratibu gani wa kuwaingiza wafanyabiashara wengine' Amesema Sheilla.
Aidha amesema atahakikisha mara baada ya kukamilika kwa mradi huo, wafanyabiashara waliosaini mikataba ya awali kabla ya ujenzi kuanza ambao walikuwa katika Soko la zamani wanapewa kipaumbele kufanya biashara katika soko hilo.
Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, Mhe. Pascal Kihanga, ameishukuru LAAC na kusema wamefanya jambo zuri kutembelea mradi huo.
Amesema, kitendo cha LAAC kutembelea miradi mbali mbali kinasaidia kuzimulika Manispaa na kuonesha jinsi utekelezaji wa miradi inavyotekelezwa pamoja na kuona thamani ya fedha inavyotumika .
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa