Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro imeendelea kutoa huduma mbalimbali zenye lengo la kuzuia maambukizi mapya ya Virusi vya Ukimwi (VVU) na kupunguza vifo vitokanavyo na Ukimwi na mafanikio ya utekelezaji huo ni kupungua kwa kiwango cha maambuzi kutoka asilimia 5.4 mwaka 2016 hadi asilimia 4.9 Septemba mwaka huu 2018.
Mratibu wa Kudhibiti Ukimwi wa Manispaa ya Morogoro, Upendo Elias alisema hayo kupitia taarifa yake ya siku ya ukimwi Duaniani Desemba Mosi ,mwaka huu ambapo kwa Manispaa hiyo ilifanyika uwanja wa shule ya Msingi Kiwanja cha Ndege na kauli mbiu ilikuwa ni ‘ Ijue hali yako, Pima Jitambue Ishi”.
Katika maadhimisho hayo mgeni rasmi alikuwa ni Mkuu wa wilaya ya Morogoro, Regina Chonjo , ambapo Mratibu wa kudhibiti UKIMWI Manispaa alisema, katika halmashauri kuna vituo vya kutolea huduma ya upimaji wa VVU 50 na vya kutolea dawa za ARV ni 11.
Mratibu huyo alisema , kupungua huko kunatokana na elimu iliyotolewa na kuendelea kutolewa kuhusu mambo ya msingi ya VVU na Ukimwi kwa jamii na jinsi ya kukabiliana na athari zitokanazo na Ukimwi.
Alisema , kuanzia Januari hadi Septemba mwaka huu jumla ya waliojitokeza kupima VVU walikuwa ni 65,178 kati yao wanaume ni 25,307 na wanawake ni 39,871 na waliokutwa na maambukizi ni 3,213 kati yao wanaume ni 1,039 na wanawake 2,174 ambayo ni sawa na asilimia 4.9
Pamoja na hayo Mratibu wa Kudhibiti Ukimwi wa Manispaa ya Morogoro alisema , mwaka 2017 jumla ya waliopimwa walikuwa 75,549 wakiwemo wanaume 26,862 na wanawake 48,687 na waliokutwa na maambukizi walikuwa 3,593 wakiwemo wanaume 1,182 na wanawake 2,411 ambayo ni sawa na asilimia 4.8
Kwa huduma za kuzuia maambukizi ya kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto alisema , akina mama wajawazito 21,467 walipima VVU na akina mama 475 walipatikana na maambukizi mbapo ni sawa na asiklimia 2.2 .
“ Wajawazito wote waliopatikana na maambukizi walipatiwa huduma ya kuzuia maambukizi ya kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto” alisema Upendo.
Pamoja na hayo alisema , takwimu hizo zinaonesha kuwa maambukizi ya ukimwi bado yako juu kwa watu waliopima katika halmashauri ya Manispaa na wanawake inaonesha wameambukizwa zaidi ukilinganisha na wanaume.
Pia alisema kuibuka kwa kasi ya ongezeko la makundi maalumu yenye tabia hatarishi zinazosababisha kuongezeka kwa maambukizi ya VVU ni pamoja na kundi linalofanya biashara ya ngono na baadhi ya watumia dawa kutoweka wazi hali zao .
Naye Mkuu wa wilaya hiyo, Chonjo kwenye hotuba yake aliwataka wanaume wa wilaya hiyo kujitokeza kwenda kupima afya zao badala ya kuwaacha wanawake ama wake wao wakiwa mstari wa mbele kupima afya na hiyo inaokana na idadi yao kitakwimu kuwa ndogo.
Hata hivyo licha ya serikali kuendelea kuchukua hatua mbalimbali ya kudhibiti , lakini ,ugonjwa upo ndani ya jamii hasa mijini kutokana na kuishi kwa mazoea bila kuchukua tahadhari jambo linaloendeleza maambukizi ya ukimwi
Mkuu wa wilaya aliitaka jamii kuendelea kuwahudumia watu wenye kuathirika na UKIMWI kwa kuacha kuwanyanyapaa , kuwatunza watoto yatima na wenye kuishi katika maisha hatarishi ili waone wao ni sehemu ya jamii.
Kwa upande wake Meya wa Manispaa, Pascal Kihanga aliwataka wakazi wa Manispaa kuendelea kuchukua tahadhari ya kujikinga na maambukizi mapya ya UKIMWI hasa ikizingatia Manispaa inapitiwa na barabara nyingi za kwenda mikoani na pia mwingiliano wa shughuli za kimaendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa