Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais , Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, (TAMISEMI) Sulemani Jafo amewaagiza wakurugenzi wote wa halmashauri nchini ambazo zinaendelea kujenga miradi ya kimkakati ya masoko na vituo vya mabasi kuhakikisha inajengwa kulenga mahitaji ya wafanyabiashara wote na kutoa kipaumbele cha kwanza kwa waliokuwepo awali kabla ya miradi hiyo.
Waziri Jafo alitoa agizo hilo wakati alipofanya ziara ya ukaguzi wa ujenzi wa soko jipya la kisasa la Manispaa ya Morogoro hivi karibuni mara baada ya Serikali kuu kutoa fedha Sh bilioni 17.6 .
Alisema ,kwa sasa Serikali ya awamu ya tano imetoa Sh bilioni 146 kwa miradi 22 ya aina hiyo katika halmashauri mbalimbali nchini ,lengo ni kuzifanya halmashauri zijitegemee kwa njia ya mapato na kujiimalisha kiuchumi .
Jafo alisema , baada ya kutolewa kwa fedha hizo , anao wajibu wa kufanya ziara ya kikazi ya kukagua na kujilidhisha utekelezaji wa miradi hiyo kuanzia mkoa wa Dar es Salaam pamoja na Morogoro ambapo ujenzi wa soko la kisasa unafanyika .
“ Rais wetu anayo malengo ya kuziwezesha halmashauri zetu zikuwe kiuchumi kupitia vitenga uchumi vyake ikiwemo ya kujengwa kwa masoko mapya ya kisasa likiwemo la la Manispaa ya Morogoro” alisema Jafo.
Hivyo alitumia fursa hiyo kutoa agizo kwa wakurugenzi wote wa halmashauri kuwa patia sehemu za kufanya biashara ‘vizimba ‘ wafanyabaishara wadogo ambao waliopisha maeneo ya masoko ya zamani kuwezesha ujenzi wa masoko mapya ya kisasa.
“ Hapa halmashauri ya Manispaa orodhesheni majina ya wafanyabiashara waliokuwepo zamani na kupisha ujenzi ili mara baada ya kukamilika wawe wa kwanza kupata maeneo na si kuwanufaisha wafanyabiashara wakubwa ama viongozi wa serikali wenye uwezo …hili nalitoa kama agizo kwa nchi nzima “ alisema Jafo.
‘ Si kwamba hatukatai hawa wafanyabiashara wakubwa wasifanye biashara ila kipaumbele kiwe ni wa wafanyabiashara wadogo na mama lishe wakitengewa maeneo yao” alisema Jafo.
Akizungumzia ujenzi wa soko hilo, Waziri huyo aliwasifu wakandarasi kwa kuonesha uwezo wao kwa maandalizi ya awali ya ujenzi na kuwaagiza kujenga soko hilo kwa kuzingatia viwango vya ubora kwa kuwa ni fedha nyingi zimetegwa kwa ajili hiyo.
Hata hivyo aliwahakikishia kuwa , Serikali itawalipa kwa wakati fedha zinapokuwa zinahitajika kwa ajili ya kuendelea na ujenzi hadi kufikia kukamilishwa kwake ifipako Augosti 2019.
Naye Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, John Mgalula katika taarifa yake kwa Waziri Jafo alisema kuwa eneo la ujenzi wa soko lina ukubwa wa mita za mraba 23, 432 ambapo fedha hizo zimetolewa na Wizara ya Fedha kupitia hazina .
Alisema , soko hilo lenye ghorofa mbili litakapokamilika litakuwa na uwezo wa kuchukua wafanyabiashara zaidi ya 2,000 na ujenzi wake unafanyiwa na Kampuni ya Uhandisi na ujenzi ya Nandhra ambao ilishinda zabuni na kuingia mkataba wa ujenzi .
Kwa upande wake ,Meneja wa mradi huo kutoka Kampuni ya Uhandisi na Ujenzi ya Nandhra , Rabinder Singh alimhakikishia waziri huyo kuwa watafanya kazi kadiri ya uwezo wao kwa kushirikiana na timu ya Manispaa pamoja na msimamizi na Mshauri wa mradi huo kukamilisha ujenzi huo kwa muda wa miezi 12 kama ulivyopangwa.
Soko jipya linalojengwa ni la kisasa na lenye ghorofa mbili kwa ajili ya matumizi ya wafanyabiashara wa aina mbalimbali na kujengwa huko ni baada ya soko la zamani iliyojengwa mwaka 1953 lilivunjwa miaka miwili iliyopita kutokana na uchakavu mkubwa.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa