SERIKALI imetenga kiasi cha Sh trilioni 1.15 kwa ya matumizi ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu mbalimbali ya shule za msingi zilizochakavu kupitia Mradi wa Kuimarisha Elimu ya Awali na Msingi (BOOST), katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka huu wa fedha.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais ,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa,(TAMISEMI) Angellah Kairuki, alisema hayo Januari 9, 2023 mjini Morogoro wakati akifungua kikao kazi cha mapitio ya tathimini ya utekelezaji wa shughuli za uboreshaji na usimamizi wa elimu kwa mwaka 2022 na mpango mwaka 2023.
Mpango wa ujenzi na ukaratabi wa miundombinu ya shule hizo unatarajia kuanza kutekelezwa Januari na Februari mwaka huu nchini kote.
Waziri alisema kuwa baadhi ya shule zitavunjwa na kujengwa upya ,nyingine zitafanyiwa ukarabati mkubwa pamoja na mdogo kwa lengo la kuzifanya ziwe na mazingira bora kulingana na hali ya sasa kwa walimu na wanafunzi.
Alisema Serikali inatambua shule nyingi ni za muda mrefu ambazo zilijengwa na Serikali, wadau na wazee na nyingine kwa njia ya kujitolea ambazo zimeweza kudumu kwa muda mrefu na imefika wakati sasa wa kuziboresha shule hizo.
Waziri alisema katika kuendelea kuimarisha elimu ya Sekondari kupitia mradi wa SEQUIP, ambapo Jumla ya sh trilioni 1.2 zitatumika kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya 1,026 ( Za kata 1,000 na za bweni za wasichana za Mkoa 26) katika kipindi cha miaka mitano.
Waziri huyo alisema mwaka 2021 jumla ya shule mpya 232 za sekondari za Kata zimeshajengwa na 10 za bweni za wasichana za mikao zinaendelea kukamilisha ujenzi wake.
Alisema kwa mwaka 2022/23, Serikali inategemea kujenga shule mpya za Kata 184, moja kila Halmashauri na shule tano (5), za bweni za wasichana kwenye mikoa mitano.
Waziri pia alisema kuanzia Januari hadi Juni mwaka huu Serikali itatoa sh milioni 600 kwa ajili ya ujenzi wa shule moja ya sekondari kwa kila Halmashauri nchini
“Nitumie fursa hii kumshukuru na kumpongeza Mhe. Dk Samia Suluhu Hassan kwa jitihada kubwa hizi anazoendelea kuzifanya katika kuimarisha na kuboresha sekta ya Elimu nchini” alisema Kairuki
Kwa upande uandikishwaji wa wanafunzi wa darasa la awali na msingi nchini aliagiza watendaji wa sekta ya elimu , wakurugenzi wa Halmashauri , wakuu wa wilaya na mikoa kuongeza kasi ya kusajili wanafunzi ili kufikia malengo ya yaliyokusudiwa ya asilimia 100 .
“Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa muendelee kuhamasisha uandikishaji wa wanafunzi wa elimu ya awali na msingi ili kuhakikisha mnafikia malengo ya uandikishaji mliyokuwa mmejiwekea” alisema Waziri Kairuki
Waziri Kairuki alisema “Kila kiongozi akahakikishe anaimarisha uwajibikaji wa watumishi wote katika ngazi zote ili kuongeza tija katika utendaji wa kazi” alisisitiza Waziri
Hivyo alisema natarajia kuanzia Januari 2023 kutakuwa na mabadiliko makubwa katika usimamizi wa elimu msingi na sekondari katika shule zetu.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Elimu Tamisemi, Vicent Kayombo alisema utekelezaji wa sera ya elimu bila ada imeongeza idadi ya wanafunzi wanaosajiliwa kujiunga elimu ya awali, msingi na sekondari nchini
Kayombo alisema bado zipo changamoto kadhaa ikiwemo kwa wanafunzi wanao maliza darasa la saba hawajui kusoma, kuandika na kuhesabu huku kukiwa na wanafunzi asilimia 20 wanaoshindwa kufaulu mtihani wa elimu ya msingi na kushindwa kujiunga na kidato cha kwanza.
Pia alisema kumekuwepo na idadi ndogo kwa wanafunzi wanaofaulu mtihani wa kidato cha nne kwa daraja la kwanza hadi tatu likiwemo somo la Kiingereza .
Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Morogoro, Fatma Mwassa,katika taarifa yake kwa Waziri alisema kuwa ,wanafunzi walioandikishwa darasa la awali na msingi hadi kufikia Januari 6, mwaka huu walifikia 74,578 kati ya hao wavulana 37,342 na wasichana 37578 sawa na asilimia 94.5 .
Mwassa alisema miongoni mwa wanafunzi hao ni wakiwemo wenye mahitaji maalum na kwamba hali ya uandikishaji bado inaendelea katika shule zote katika mkoa wa Morogoro.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais ,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa,(TAMISEMI) Angellah Kairuki, akizungumza na Watendaji wa Idara ya Elimu ngazi ya mkoa na Halmashauri Januari 9, 2023 mjini Morogoro wakati akifungua kikao kazi cha mapitio ya tathimini ya utekelezaji wa shughuli za uboreshaji na usimamizi wa elimu kwa mwaka 2022 na mpango mwaka 2023.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa