Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameziagiza halmashauri zote nchini kuendelea na kazi ya kupima ardhi za makazi na mashamba na kutoa hati ili wananchi wazitumie kupata mikopo na kuonya kuwa serikali haitasita kuchukua hatua kwa maafisa watakao hujumu ugawaji wa mashamba pori kwa wakulima kwa manufaa yao binafsi.
Pia ameuagiza Wakala wa Vipimo nchini kwa kushirikiana na halmashauri zote kuendesha msako wa vipimo maalumu ili kuwachukulia hatua wafanyabiashara wanaotumia vipimo vya lumbesa kununua mazao ya wakulima kwa vile ni unyonyaji na kuwataka MVIWATA kuisaidia serikali katika hilo.
Waziri Mkuu alitoa maagizo hayo katika hotuba yake ya kufungua maadhimisho ya miaka 25 ya Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania ( MVIWATA) jana kwenye uwanja wa Jamhuri wa mjini Morogoro.
Waziri Mkuu aliyekuwa mgeni rasmi katika ufunguzi alimwakilisha Rais Dk John Magufuli ambapo pia Waziri wa Kilimo, Dk Charles Tizeba alishiriki kwenye ufunguzi huo na kumkaribisha waziri mkuu.
“ Wakala wa vipimo endesheni oparesheni ya kukamata mfanyabiashara yoyote anayebeba lumbesa na shirikianeni na halmashauri , hatuwezi kuruhusu wizi wa rejareja …fanyeni kazi yenu na nitapita huko kujua kwanini lumbesa bado ipo “ alisema Waziri Mkuu Majaliwa.
Hata hivyo alisema, Serikali ya awamu ya tano inatambua umuhimu wa wakulima wadogo na mchango wao katika uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara , hivyo itaendelea kushirikiana nao kupitia Vikundi vyao ya ushirika ikiwemo MVIWATA.
Waziri mkuu lisema , mpango wa sasa ni kuona mazao yanalimwa kitaalamu kwa kufuata ushauri wa watalamu wa kilimo na ili kufanikisha jambo hilo , Serikali kupitia wizara ya kilimo itaendelea kusambaza pembejeo na mbolea kwa wakati kwa wakulima nchini .
Hata hivyo alisema , katika utekelezaji wa serikali kwenye sekta ya kilimo kiasi cha sh: bilioni 56.45 zimetolewa kwa ajili ya mikopo ya kilimo kupitia Benki ya Mendeleo ya Kilimo hasa katika zao la kahawa na mahindi kwa wanufaika 527,000 katika mikoa 13 nchini na upelekaji wa tani milioni 2.2 za mbolea na dawa maeneo ya wakulima vijijini.
Waziri mkuu pia alitioa agizo kwa Waziri wa Viwanda , Biashara na Uwezeshaji , Charles Mwijage kufika kushiriki kwenye kongamano ya wakulima wa MVIWATA kusikiliza kero zao kwa lengo la kuzifanyia kazi kuagiza watendaji wa wizara husika za kilimo, ardhi na kutaka benki zote kushiriki kongamano litakalofanyika mjini Morogoro .
Alisema , lengo ni kushiriki kujadili masuala mbalimbali ya wakulima ili waweze kuishauri serikali namna ya kukabiliana na changamoto hizo wakiwemo na Wakurugenzi wa watendaji wa mabenki yanayohusika na utoaji wa mikopo.
Naye Mwenyekiti wa MVIWATA, Abdul Gea alimweleza Waziri mkuu juu ya changamoto ya bei ya mazao kuendelea kushuka chini tangu msimu wa mwaka 2017/2018 na bado mazao mengi yapo magharani hali inayochangia wakulima kuendelea kuwa maskini licha ya kuongeza kiwango cha uzalishaji wa mazao .
Hata hivyo alisema , wakulima wanayo imani ya serikali ya awamu ya tano kuweza kusaidia kupata masoko ya uhakika na wenye bei nzuri kwa ajili ya kuua mazo yao .
Mkurugenzi Mtendaji wa MVIWATA, Stephen Ruvuga alisema, kongamano la kitaifa la wakulima lenye mada inayohusu “ujenzi wa uchumi wa viwanda nini nafasi ya wakulima wadogo” limeshirikisha wanachama zaidi ya 2,400 kutoka mikoa ya Tanzania Bara na Visiwani.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa