Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, mheshimiwa Adam Malima ametoa shukurani sana kwa vijana 33 waliojitolea kuokoa wananchi waliokumbwa na mafuriko tarehe 24.01.2024 kwenye Kata ya Kihonda, Manispaa ya Morogoro.
Shukurani hiyo iliyoambatana na fedha kiasi cha shilingi milioni moja laki nane (1,800,000) ameitoa leo, tarehe 05.02.2024 kwenye uwanja wa Ofisini kwake, alipokutana na vijana hao wakiwa wameambatana na Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Mkoa wa Morogoro.
“Mlichokifanya siku ile binafsi yangu nilifarijika sana maana mlichangia sana kuokoa maisha ya watanzania wenzetu.
Pia nimefarijika tena kuona kwamba baada ya tukio lile vijana wengine wamehamasika kuungana nanyi na sasa idadi yenu nimeambiwa imefika 75” alieleza Malima.
Mheshimiwa Malima amesema kwamba kwa kushirikiana na Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Mkoa wa Morogoro, watawasiliana na Ofisi ya Zimamoto Makao Makuu waweze kuandaa mafunzo rasmi ya wiki mbili kwa vijana hao ili kuwajengea uwezo zaidi wa uokoaji.
“Ofisi yangu itagharamia mafunzo hayo na nitatafuta wadau wengine watuunge mkono katika hili maana tunataka kikosi chenu kiwe cha vijana wa mfano nchini” aliongeza kusema Malima.
Aidha, mheshimiwa Malima amesema vijana watakaopenda kujiunga na kikosi hicho cha uokoaji wawe ni wenye nidhamu, utayari, maadili mema, na wanaojua kwamba kazi hiyo ya uokoaji ni ya kujitolea.
Naye mwakilishi wa vijana hao, ndugu Salum Selemani amemshukuru sana Mkuu wa Mkoa kwa zawadi aliyowapatia na kuahidi kuendelea kushiriki katika shughuli za uokoaji kila itakapobidi.
Pia ametoa wito kwa wananchi kuendelea kuchukua tahadhari na kutoa taarifa kupitia namba ya simu ya dharula 114, pindi wanapokuwa wamefikwa na majanga na kuhitaji msaada.
MWISHO
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa