Kamati ya Fedha na Uongozi ya Halmashauri ya Manispaa Morogoro ikiongozwa Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo, mheshimiwa Pascal Kihanga, wameridhia kujenga shule ya msingi ya dharula kwenye eneo la shule ya sekondari Tushikamane kwenye Kata ya Lukobe, ikiwa ni jitihada ya Manispaa ya kuhakikisha wanafunzi wa shule ya msingi Juhudi wanaendelea na masomo yao baada ya shule yao kufungwa hivi karibuni kwa ajili ya usalama wa wanafunzi na walimu dhidi ya mafuriko ambayo yametokea mara kadhaa shuleni hapo katika kipindi hiki cha mvua.
Ridhaa hiyo imekuja mara baada ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, ndugu Ally Machela kuwasilisha ombi la ujenzi huo, ambapo alisema Kamati yake ya Wataalamu (CMT) pia wamesharidhia na hivi sasa wanasubiri kibali kutoka Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Morogoro ndipo ujenzi uanze haraka ili ndani ya siku tano ujenzi uwe umekamilika na wanafunzi waanze kutumia madarasa hayo.
“Kiuhalisia, panahitajika madarasa zaidi ya 20 ili kukidhi uhitaji kwa sababu shule ya Juhudi ina wanafunzi zaidi ya 1600. Lakini kwa kuwa ni dharula, tutajenga madarasa kumi ya dharula na vyoo vya dharula kwa ajili ya wanafunzi wa darasa la kwanza hadi la tano, tutakamilisha maboma mawili kwa ajili ya wanafunzi wa darasa la awali na Ofisi ya walimu.
Tunataka baada ya kupata ruhusa ya kuendelea na ujenzi kutoka Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, tupeleke timu kubwa pale chini ya wahandisi wetu ili ndani ya siku tano ujenzi uwe umekamilika na watoto wetu waweze kwenda kuendelea na masomo yao” ameeleza Machela.
Tarehe 25.01.2024, shule ya msingi Juhudi, iliyopo kwenye Kata ya Lukobe ilizingirwa na maji yaliyotokana na mvua kubwa iliyonyesha siku hiyo. Hali hii ilipelekea Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Morogoro, ambaye pia ndiye Mkuu wa Wilaya hiyo, mheshimiwa Rebecca Nsemwa kuifunga shule hiyo ikiwa ni tahadhari dhidi ya madhara yanayoweza kutokea tena kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.
MWISHO
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa