HALMASHAURI ya Manispaa ya Morogoro imepanga kutumia kiasi cha Sh bilioni 1.1 kwa ujenzi wa Sekondari maalumu ya ghorafa mbili katika kata ya Boma kwa kutumia fedha za mapato ya ndani .
Shule hiyo mpya ya ghorofa mbili ikiwa na vyumba vya madarasa 15, ofisi za walimu pamoja na mkuu wa shule imeanza kujengwa kuanzia mwaka wa fedha wa 2021/2022 katika kata hiyo kutokana na kuwa eneo dogo la ardhi na hadi sasa zimetumika Sh milioni 650 kwenye ujenzi huo.
Mkurugenzi wa Manispaa Ndg. Ally Machela alisema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea kuona miradi ya sekta ya elimu inayotekelezwa na kusimamiwa na Manispaa ukiwemo ujenzi wa shule mpya ya ghorafa mbili
“ Mradi huu unakisiwa kutumia kati ya Sh milioni 800 hadi Sh bilioni 1.1 hadi utakapokamilika na hivi sasa umeshatumia kiasi cha Sh milioni 650 hadi ulipofikia ikiwa ni pamoja na ununuzi wa vifaa “ alisema Machela
Alisema kwa sasa ujenzi umefikia hatua ya upauaji na ujenzi wake unatarajia kukamilika mwaka huu wa fedha wa 2022/2023 kwa asilimia 100 na kuwezesha wanafunzi wa kata hiyo ifikapo Januari , 2023 kuwa madarasani.
“Tumepata mawazo mbalimbali ya wadau wakishauri iwe sekondari maalumu kwa ajili ya watoto wa kike na wengine kushauri iwe ni sekondari maalumu ya mchepuo wa masomo ya sayansi “ alisema Machela
Mbali na fedha za mapato ya ndani alisema , Manispaa yenye kata 29 bado nyingine hazina shule za sekondari ,lakini mwaka uliopita zimejengwa shule mpya nne kwa gharama ya Sh bilioni 1.7 .
Machela alisema shule hizo zimejengwa kutokana na fedha za Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Covid – 19.
“ Shule hizi mpya tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia fedha za madarasa 86, lakini katika mdarasa 40 tuliamua kuanzisha shule mpya kwa maana ya sekondari mpya katika kata ya Mbuyuni, Tungi , Mkundi na Mazimbu na tayari zimesajiliwa na wanafunzi wa kidato cha kwanza wameanza masomo” alisema Machela
Katika hatua nyingine alisema , Manispaa hiyo ilipokea fedha Sh milioni 940 kati ya bilioni 1.2 kutoka serikali kuu kupitia Mradi wa Kuboresha Mazingira ya Kufundishia na Kujifunzia kwa Elimu ya Sekondari (SEQUIP) .
Alisema fedha hizo zimetumika kwa kujengwa shule mbili mpya za sekondari katika kata ya Mindu na Lukobe na kila moja ilipewa Sh milioni 470 ambapo vyumba 16 vya madarasa yamekamilika.
Machela alisema ,ujenzi huo umehusisha maabara sita , maktaba mbili , vyumba vya Tehama ,majengo mawili ya utawala na matundu 40 ya vyoo na kwamba majengo hayo yamepauliwa na kuezekwa , kupingwa rangi na hatua nyingine za umaliziaji.
Kwa uande wake Meya wa Manispaa hiyo , Pascal Kihanga alisema kwa mwaka wa fedha 2022/23 imepanga kukamilisha miradi ya maendeleo na kutoa mikopo ya asilimia 10 kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Naye Ofisa Taaluma Sekondari wa Manispaa hiyo, Herieth Kagosi alisema uboreshwaji wa miundombinu ya elimu na ujenzi wa shule mpya kunaifanya Manispaa kujipanga kuboresha taaluma ya elimu na kufuta ziro katika shule zake 27 za sekondari zilizopo .
Kwa upande wake Mwenyekiti wa mtaa wa Mindu Shomari Ahuman alisema baada ya kujengwa kwa shule ya sekondari katika kata yao , wananchi wamejipanga kushiriki kikamilifu kusaidia ujenzi wa nyumba za walimu baada ya serikali kuu kutoa fedha .
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa