Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro imetenga kiasi cha Sh milioni 10 kwa ajili ya matumizi ya upatikanaji wa vitambulisho vya wazee vitakavyowawezesha kupatiwa huduma mbalimbali zikiwemo za matibabu bure .
Pia halmashauri imeandaa vitambulisho vya wazee 4,002 kati ya hivyo wanaume 1,521 na wanawake 2,481 sambamba na kuwalipia wazee 3,378 bima ya Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF iliyoboreshwa) wakiwemo wanaume 1,462 na wanawake ni 1,416 .
Kaimu Mganga wa Manispaa ya Morogoro , Vulfrida Kyara, alibainisha hayo kwenye kongamano la siku ya kuelimishana kupinga ukatili dhidi ya wazee Duniani ambapo kauli mbiu yake ni “ Tuungane Kupaza Sauti ya Wazee 2019”.
Kongamano hilo ngazi ya Manispaa ya Morogoro ambalo liliandaliwa na Shirika la kusaidia Wazee mkoa wa Morogoro (MOREPEO), kwa kushirikiana na Shirika la kimataifa la HelpAge.
Hata hivyo Kaimu Mganga mkuu wa Manispaa alisema , licha ya vitambulisho hivyo kudumu kwa muda wa mwaka mmoja , wazee wamekuwa wakipewa kipaumbele cha kwanza wanapofika kupata matibabu kwenye zahanati na vituo vya afya.
Katika hatua nyingine , Kyara aliungana na wazee wa Manispaa juu ya changamoto ya walioko kwenye Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya,(NHIF), kwa kushindwa kupata dawa katika vituo vya afya licha ya sasa vina madaktari wenye uzoefu.
“ Kwa sasa kuna maboresho makubwa ya huduma za afya zinazotolewa na Serikali na Vituo vya Afya vimeboreshwa na vina madaktari wa magonjwa tofauti ambao wanauwezo wa kutoa dawa ,lakini mgongwa mwenye NHIF hawezi kupata dawa alizoandikiwa hata kama kituo kina daktari mbobezi” alisema Kyara.
Nao wazee hao waliiomba Serikali kupitia upya Sera ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kwa kuzingatia namna orodha ya magonjwa na dawa zinapaswa kutolewa kuanzia ngazi ya zahanati, kituo cha afya na hospityali na hasa ngazi ya vituo vya afya kwa vile sasa vina madaktari wengi tofauti na huko nyuma.
Katibu mkuu wa Baraza la Wazee wilaya ya Morogoro, Dk Bakil Anga licha ya kuipongeza Serikali kwa juhudi kubwa inazoendelea kufanya ili kuhakikisha maisha ya wazee wote nchini yanakuwa bora na salama zaidi alitaka mkakati endelevu wa uundwaji wa mabaraza ya wazee yawe jumuishi na TAMISEMI.
Naye Mkurugenzi wa MOREPEO, Samson Msemembo alisema ,wazee wanakabiliwa na changamoto nyingi hasa katika huduma za afya hivyo ameziomba mamlaka husika kuwasaidia kwa karibu zaidi.
Kwa upande wa Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro ,Pascal Kihanga pamoja na Afisa maendeleo ya Jamii na vijana Manispaa Enedy Mwanakatwe kwa nyakati tofauti wamesema, serikali inaendelea kuweka mifumo mizuri ili kuhakikisha wazee wote wanaendelea kupata huduma bora.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa