MKUU wa mkoa wa Morogoro Dk Kebwe Stephen Kebwe ameiagiza halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kuhakikisha hoja zote za Mdhitibi na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ambazo hazijajibiwa kwa muda mrefu zinajibiwa.
Pia ameitaka halmashauri kuhakikisha , inawasilisha hesabu zinazoishia Juni 30, 2018 kabla ya Septemba 30, mwaka huu ili ziweze kukaguliwa .
Mkuu wa mkoa ametoa agizo hilo baada ya Meya wa Manispaa hiyo, Pascal Kihanga kufungua kikao maalumu cha baraza la madiwani wa halmashauri kupitia majibu ya hoja za ukaguzi za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka 2016/2017.
Dk Kebwe aliitaka halmashauri ihakikishe kuwa inadai madeni yake yote toka kwa wadaiwa ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua za kisheria kwa wadaiwa sugu ili kuongeza mapato ya ndani ya halmashauri ya Manispaa.
Pia alitaka kuhakikisha inapeleka fedha za miradi ya maendeleo kwa wakati ikiwa na pamoja na fedha a mfuko wa Jimbo zinazotolewa kwa wabunge.
“ Kutopeleka fedha za miradi ya maendeleo kwa wakati kunasababisha halmashauri kuonekana inashindwa kufanya matumizi ya fedha hizi na miradi kutokamilika kwa wakati , hivyo kupunguza imani ya wananchi kwa Serikali yao” alisema Dk Kebwe.
Mkuu wa mkoa pia alisisitiza kuwa kitengo cha ukaguzi wa ndani kiwezeshwe ipasavyo ili fedha zote za miradi zikaguliwe kwa wakati na thamani ya fedha ionekane .
Dk Kebwe aliitaka halmashauri kulipa asilimia 10 ya fedha za wanawake , Vijana na watu wenye ulemavu kutoka katika mapato yake ya ndani kiasi cha Sh 318,164,055 sambamba na kulipa malimbikizo ya madeni ya nyuma.
Mkuu huyo wa mkoa alisema, taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha wa 2016/2017 inaonesha kuwa , mkoa wa Morogoro umefanya vizuri kwa taasisi zake pamoja na halmashauri zote tisa za mkoa kwa kupata hati safi .
Naye Mkaguzi mkuu wa Nje Mkoa wa Morogoro, Mwabwanga Andindilile alisema, pamoja na kupata hati safi , bado madiwani wanalo jukumu la kuhakikisha wanasimamia vyema ukusanyaji wa mapato na kufuatilia matumizi yake ili kuona miradi ya maendeleo inakamilishwa kwa wakati .
kwa upande wake , Meya wa Manispaa hiyo, Pascal Kihanga alimhakikishia mkuu wa mkoa kuwa Baraza hilo kwa kushirikiana na wataalamu litazifanyia kazi hoja hizo ili ziweze kujibiwa na kuiwezesha halmashauri kuendelea kupata hati safi .
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa