Wizara ya fedha imeipatia halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kiasi cha Sh bilioni 18 .1 kwa ajili ya ujenzi wa soko jipya na la kisasa la ghorofa mbili kwa ajili ya matumizi ya wafanyabiashara wa aina mbalimbali baada ya soko la zamani lililojengwa mwaka 1953 kuvunjwa miaka miwili iliyopita.
Meya wa Manispaa ya Morogoro, Pascal Kihanga alisema hayo Augosti 29 wakati wa makabidhiano ya eneo la ujenzi wa soko jipya la kisasa na Kampuni ya Uhandisi na ujenzi ya Nandhra ambayo ilishinda zabuni na kuingia mkataba wa ujenzi wa soko hilo.
Alisema , fedha hizo zimetolewa na Wizara ya fedha ikiwa ni utekelzaji wa ahadi ya Rais Dk John Magufuli aliyoitoa kwa wananchi wa Manispaa hiyo alipofanya ziara mapema mwezi Mei mwaka huu alipokuja kufungua stendi ya kisasa ya mabasi ya Msamvu .
Kihanga kwa niaba ya wananchi wa Manispaa alimshukuru Mh.Rais na kusema kuwa ujenzi wa soko hilo ni miongoni mwa miradi endelevu itakayoiingizia mapato yatakayosaidia kuboresha huduma za kijamii.
“ Kwa Manispaa ya Morogoro ni siku nzuri sana , kinachofanyika leo ni muhimu kwetu na taifa … fedha hizi zimetolewa na Rais , umuhimu huu utaonekana wakati wa ujenzi na ubora wa majengo na muda muafaka utakaotumika kukamilisha ujenzi huu” alisema Kihanga na kuongeza kusema .
“ Zoezi la leo ( Aug 29) ni kumkabidhi eneo mkandarasi kwa ajili ya kuanza ujenzi wa soko kwani Serikali imetoa fedha zote “ alisema Kihanga .
Hata hivyo alimwomba mkandarasi wa ujenzi wa soko , na Msimamizi Mshauri wa mradi huo kuifanya kazi hiyo kwa viwango vya ubora wa hali ya juu, na kumaliza kazi kwa muda wa miezi 12 kulingana na mkataba na kwamba haitakuwa dhambi endapo atamaliza ujenzi kabla ya muda huo.
Alisema , wafanyabiashara wanahamu kuona ujenzi wa soko unaisha mapema ili waweze kurudi maeneo yao ya zamani baada ya kuamishwa kupisha kuvunjwa soko liliilokuwepo ambalo lilikuwa ni hatari kwao na watumiaji wengine wa ndani na nje ya mkoa .
Kihanga alisema , mara ujenzi wake utakapokamilika kipaumbele kitawekwa kwa wafanyabiashara waliopisha ujenzi kwa kuingia nao mikataba mipya na wengineo wakiwemo wafanyabiashara wadogo wakiwemo wanawake kwa vile soko hilo litakuwa na vibanda vingi vya maduka na maeneo ya kutolea huduma mbalimbali za kijamii.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa hiyo , Michael Waluse alisema , wizara ya fedha imetoa jumla ya Sh bilioni 18.1 za kazi na kati ya fedha hizo Sh milioni 521 ni kwa ajili ya ushauri na usimamizi wa mradi na fedha halisi ya ujenzi wa soko hilo kwa malipo ya mkandarasi ni Sh bilioni 17.6 .
Waluse alisema , eneo la ujenzi wa soko lina ukumwa wa mita za mraba 23, 432 na mradi huo ni miongoni mwa miradi ya kimkakati ya Manispaa hiyo na fedha hizo zimetolewa na Wizara ya Fedha kupitia hazina ambapo ufuatiliaji wa matumizi ya fedha utakuwa ni wa karibu na kwamba kila jicho litapita kuona maendeleo ya mradi huo.
Naye Msimamizi na Mshauri wa mradi huo, kutoka Kampuni ya PSM Architects , Peter Matinde alisema tayari wamemkabidhi michoro mkandarasi wa ujenzi wa soko hilo la kisasa la Morogoro ambapo katika muda wa wiki mbili kuanzia Septemba 6, mwaka huu (2018) ni wa kukusanya vifaa vya ujenzi eneo la ujenzi.
Hata hivyo alisema kuwa, atashirikiana na viongozi wa Manispaa na mkandarasi ili kuona kazi hiyo ina kamilishwa kwa wakati na ubora unatakiwa kwa kufuata utaratibu wote wa kimkataba .
Kwa upande wake ,Meneja wa mradi huo kutoka Kampuni ya Uhandisi na Ujenzi ya Nandhra , Rabinder Singh aliwahakishia Meya wa Manispaa , viongozi na wananchi kuwa watafanya kazi kadiri ya uwezo wao kwa kushrikiana na timu ya Manispaa pamoja na msimamizi na Mshauri wa mradi huo kukamilisha ujenzi huo kwa muda wa miezi 12 kama ulivyopangwa.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa