HALMASHAURI ya Manispaa ya Morogoro imetakiwa kuweka nguvu katika kujikita kupambana na afya duni za Watoto.
Kauli hiyo imetolewa Desemba 16/2020 na Afisa Tawala Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Hilary Sagara, akimwakilisha Mkuu wa Wilaya katika maadhimisho ya Kilele cha Siku ya afya na Lishe iliyofanyika katika Zahanati ya Malipula Kata ya Chamwino Manispaa ya Morogoro.
“Niwapongeze sana Manispaa ya Morogoro kwa kushirikiana na wadau wa lishe, lakini nawapongeza sana watoa huduma ngazi ya jamii na ngazi ya Vituo vya kutolea huduma, kwakweli kwa haya niliyoyaona mmefanya kazi kubwa sana ya kuhakikisha Manispaa ya Morogoro inatokomeza watoto wenye udumavu, ombi langu endeleeni kupambana ikiwemo kutoa elimu mara kwa mara ili huduma hii iweze kutekelezeka vizuri katika Jamii”
Sagara, ameyataka Mabaraza yote ya Maendeleo ya Kata pamoja na Mitaa kujenga utaratibu wa kuwaalika watoa huduma ngazi za Jamii na vituo vya afya ili waweze kutoa elimu kwani huko ndipo chimbuko la afya ndipo linapojitokeza.
Aidha, amesema kuwa kauli mbiu ya mwaka huu ni lishe kwa maendeleo endelevu, hivyo jamii inapaswa kufanya kazi kwa bidii na kuweka mikakati mizuri ya uzalishaji wa chakula katika ngazi za Kaya ili Manispaa na Mkoa kwa ujumla kuweza kusonga mbele.
Mwisho, amewataka wajumbe wa kamati ya lishe katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro na Wilaya kwa ujumla kusimamia na kuhakikisha wanapambana na changamoto za lishe duni kwa watoto ndani ya Halmashauri.
Kwa upande wa Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro ,Dr. Ikaji Rashidi, amesema kuwa lishe duni ni suala mtambuka na Serikali kama moja ya hatua inayorudisha nyuma kimaendeleo na mapambano dhidi ya lishe duni yamekuwa ni moja wapo ya maeneo ya kipaumbele katika mpango wa pili wa maendeleo wa miaka mitano.
“kwakuwa lishe ni suala mtambuka hatuna budi kuungana na kushirikiana kwa pamoja katika kusimamia na kuhakikisha jamii yetu inaendelea vizuri, hivyo tukishirikiana kwa pamoja tatizo hilo linaweza kuepukika ” Amesema Dr Ikaji.
Hata hivyo ,Dr Ikaji, amewashauri wazazi kuhakikisha wanawapa watoto haki zao za msingi katika lishe na kwa wakinamama wanatakiwa kuhakikisha watoto wanawapa virutubisho vizuri kwa kuwanyonyesha katika kiwango cha afya na kuacha mawazo potofu ya kuofia kupoteza uzuri wao
Afisa Lishe Manispaa ya Morogoro, Elina Kweka, amesema madhumuni ya kuadhimisha siku hiyo ni kuongeza uelewa na matokeo chanya kwa jamii ili kukabiliana na changamoto za afya na lishe zinazowakabili Watoto.
Amesema changamoto za udumavu wa Watoto katika Manispaa ya Morogoro ni asilimia 26.4%, ukondefu asilimia 3.7%, unene uliozidi kwa watoto chini ya miaka 5 ni asilimia 4.1%, upungufu wa wekundu wa damu kwa wanawake walio katika umri wa kuzaa asilimia 29.8%, upungufu wa vitamin ‘A’ kwa asilimia 33, utumiaji wa chumvi yenye madini joto asilimia 64%, unawaji wa mikono asilimia 71.5% .
Kweka, amesema miongoni mwa shughuli mbali mbali za lishe zinazotolewa katika vituo vya kutolea huduma za afya zinazolenga makundi mbali mbali Wanawake, wanaume , vijana rika balehe , wadau mbalimbai , viongozi wa dini na asasi za kiraia ni pamoja na utoaji wa matone wa vitamin A, dawa za minyoo na utambuzi wa hali ya lishe kwa watoto chini ya umri wa miaka 5,
“Huduma hizi tumeanza kuzitoa kuanzia tarehe 01-31 mwezi Desemba 2020 katika vituo vyetu 47 vinavyotoa huduma za uzazi na Mtoto, huma hii hutolewa mara 2 kwa mwaka yaani mwezi wa 6 na mwezi wa 12, lakini elimu hii ya huduma tumezitoa kwa njia ya vyombo vya habari ikiwamo redio, TV , vikundi malezi vilivyopo ngazi za Mitaa, kuwaunganisha watoa huduma ngazi ya jamii katika vituo vya afya vilivyopo katika Ofisi ya Kata , utoaji wa huduma magonjwa yasiyoambukizwa yanayohusiana na lishe, elimu katika makao ya Watoto na kutoa mafunzo kwa watoa hudma na vikundi vya wakulima kwa kushirikiana na wadau’’ Amesema Kweka.
Naye , Mratibu wa mradi wa Lishe Endelevu Mkoa wa Morogoro, Mariam Mwita, amesema suala la lishe ni mtambuka hivyo jamii kwa kushirikiana na wadau mbali mbali pamoja na Serikali kuhakikisha wanajenga Vizazi vyenye watoto wenye afya na lishe bora ili kuepuka udumavu.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa