HALMASHAURI ya Manispaa ya Morogoro, imezindua mafunzo ya wawezeshaji kuhusu utekelezaji wa kipindi cha pili awamu ya tatu na uhakiki wa Kaya zinazoshiriki kwenye mpango wa TASAF.
Mafunzo hayo yamezinduliwa leo Julai 20,2020 na Mkurugenzi wa Ukaguzi wa ndani TASAF Makao Makuu, CPA-Christopher Sanga, kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Manispaa.
Akizungumza na Waandishi wa habari, Sanga, amesema mafunzo hayo ni kujenga uwelewa wa pamoja na namna zoezi hili la uhakiki wa walengwa ambayo ni ya kwanza katika utekelezaji wa kipindi cha pili cha Awamu ya tatu ya TASAF ambacho kilizinduliwa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mwezi Februali 2020.
Sanga , amesema tathimini ya kipindi cha kwanza cha Awamu ya Tatu TASAF inaonyesha kwamba mpango wa kunusuru Kaya zinazoshiriki kwenye mpango wa TASAF umechangia kwa kiasi kufikiwa azma ya Serikali ya kupunguza umasikini nchini.
Amesema utekelezaji wa kunusuru mpango wa Kaya Masikini pia umewezesha Kaya za Walengwa kujikita kwenye shughuli za kukuza kipato na kijiimarisha kiuchumi ikiwemo Ufugaji, uvuvi, kilimo, na biashara ndogondogo.
Aidha, amesema pamoja na mafanikio hayo Vijiji/Mitaa/ Shehia zilizofikiwa katika kipindi cha kwanza ni asilimia 70% ya Vijiji/Sheria/ Shehia vyote nchini hivyo bado kuna wananchi wanaoishi katika hali duni kwenye maeneo ambayo hayakufikiwa.
“Wakati wa uzinduzi wa kipindi hiki cha pili, Mhe. Rais Dkt John Pombe Magufuli, aliagiza kwamba kabla ya shughuli zozote za kipindi cha pili kuanza, uhakiki wa walengwa ufanyike kote nchini ili kuondoa Kaya za walengwa ambazo zimepoteza sifa, mtakumbuka hapo nyuma kumekuwa na malalamiko mengi kuhusu mpango kuwa na watu wasiostahili wakiwemo watu wasio kuwa masikini, Viongozi, orodha ya walengwa kuwa na watu waliohama au waliofariki ambao hao wote waliitwa walengwa hewa, ili kutekeleza agizo la Mhe. Rais na pia kuondoa dhana iliyojengeka kwa jamii ya kuwemo walengwa hewa, tutaanza uboreshaji kwa kusafisha daftari leo la walengwa”Amesema CPA Sanga.
Amesema kipindi cha pili cha Awamu ya Tatu ya TASAF ,kitafikia Kaya Milioni moja na laki nne na nusu zenye jumla ya watu zaidi ya Milioni 7 Kote nchini hii ikiwa ni nyongeza ya Kaya laki tatu na nusu ambapo mkazo mkubwa utakuwa ni kuwezesha Kaya zitakazoandikishwa kwenye mpango kufanya kazi kufanya kazi ili kuongeza kipato.
‘”Tunataka kuwa na orodha Halisi ya Walengwa kwenye Masijala ya Kaya za Walengwa , Kaya ambayo haikufika kuchukua malipo yake mara mbili mfululizo Kaya hizo zote lazima ziondolewe” Ameongeza CPA Sanga.
Mjumbe wa Kamati ya Kitaifa ya Usimamizi wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii- TASAF, (National Steering Committee ) Eng. Rogatus Mativila, amewataka Viongozi wafanye kazi kwa uadilifu ili wafikie malengo ya Serikali kupitia kipindi cha pili cha Awamu ya Tatu ya TASAF ya kupunguza umasikini na kuchochea ukuaji wa uchumi ukiwemo ule wa Viwanda ambayo ni agenda muhimu ya Serikali.
Naye Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba, ameupongeza Uongozi wa TASAF Mkao Makuu kwa kuzindua mpango huo ambao unaongeza na kuboresha ili kutoa huduma za jamii na kuendeleza rasilimali Watoto hususani katika upatikanaji wa elimu na Afya.
Kwa upande wa Mratibu wa TASAF Manispaa ya Morogoro, Feliciana Katemana, amesema mpango huo wa kipindi cha Pili cha Awamu ya Tatu , utawezesha Kaya zote zinazoishi katika Mazingira duni zipate usaidizi wa Serikali kupitia TASAF kwa kuwawezesha kufanya kazi na kupambana na umasikini.
Katemana amesema mpango wa kipindi cha Pili cha Awamu ya Tatu ya TASAF Manispaa Morogoro umelenga kuwafikia jumla ya Walengwa 2793 katika Kata 29 ikiwamo Mitaa 164.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa