MANISPAA ya Morogoro imeingia mkataba wa miaka 15 na Mwekezaji Afro Oil Investment Ltd kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha mafuta Stendi ya Msamvu utakao gharimu kiasi cha shilingi Milioni 750 katika utekelezaji wake.
Mkataba huo umesainiwa Aprili 5/2022 katika Ofisi ya Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro huku ukishuhudiwa na pande zote mbili wakiwamo Mstahiki Meya, Mkurugenzi wa Manispaa na upande wa Ofisi ya Manunuzi Manispaa ikiongozwa na Mkuu wa Idara Jafari Makulumla , pamoja na watu kutoka Ofisi ya Mipango.
Akizungumza mara baada ya kusainiana mkataba huo, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro, Mhe. Pascal kihanga, amewataka wawekezaji kutoa taarifa na changamoto zote zinazojitokeza katika kipindi cha mchakato wa utekelezaji ili waweze kushirikiana ili kufanikisha ujenzi wa Kituo cha Mafuta unakamilika.
" Leo nimesaini Mkataba huu, muda wetu ni miezi 6 kama tulivyokubaliana , anzeni mapema ili mnufaike, matarajio yetu ni kuona ndani ya miezi 6 mkataba wetu unaanza kusoma na kituo kinafanya kazi na mnaanza kutulipa fedha zetu ili sasa kila upande uanze kunufaika maana shida yetu sio kupata fedha pekee bali tunataka kutoa huduma kwa wananchi " Amesema Mhe. Kihanga.
Naye Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Ally Machela, amemtaka mwekezaji kulipa kodi kwa wakati ili Manispaa iweze kuendesha shughuli zake mbalimbali zinazotokana na mapato hayo na vyanzo vyengine.
Kwa upande wa Mwakilishi wa Afro Oil Investment Ltd, amesema watahakikisha wanatekeleza na kuheshimu makubaliano ya mkAtaba waliosaini kwani wana uzoefu wa zaidi ya miaka 10 katika uendeshaji wa soko la Mafuta.
Upande wa Afisa Manunuzi Manispaa ya Morogoro , Jafari Makulumla , amesema mkataba huo utainufaisha Manispaa kupitia tozo za huduma mbalimbali zitakazofanywa na Afro Ltd, tozo za leseni , tozo za ukusanyaji wa taka pamoja na kutoa ajira kwa wananchi wa Manispaa ya Morogoro.
Ikumbukwe kuwa katika mchakato huo ulioanza mwishoni mwa mwaka jana 2021 na kumalizika mwanzoni mwa mwaka huu 2022, ulishindanisha washindani wawili ambao ni Afro Oil Investment Ltd na Salimu Oil Ltd ambapo katika kinyang'anyiro hicho Afro Oil Investment Ltd aliibuka mshindi.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa