HALMASHAURI ya Manispaa ya Morogoro inatarajia kukusanya kiasi cha shilingi Bilioni 10 kupitia mapato ya ndani katika mwaka wa fedha wa 2022/2023.
Hayo yamezungumzwa Februari 10, 2023, na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro, Mhe. Pascal Kihanga, wakati wa kuwasilisha rasmi Bajeti ya mwaka wa fedha wa 2022/2023 katika Mkutano maalum wa Bajeti wa Baraza la Madiwani uliofanyika katika Ukumbi wa Kilakala Soko Kuu la Chifu Kingalu Morogoro.
Akizungumza na Waandishi wa habari, Kihanga, amesema Manispaa inakadiria kukusanya na kutumia kiasi cha shilingi Tshs.84,974,512,600.00 ambapo kwenye mapato ya ndani ni Tshs.10,754,563,600.00 , ruzuku ya mishahara na matumizi ya kawaida Tshs.84,891,140,000.00 na miradi ya Maendeleo ni Tshs.8,568,986,000.00.
Hata hivyo, amesema Manispaa ya Morogoro , imeendelea na utoaji wa Mikopo ya Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu kama kanuni inavyoagiza kuwa Halmashuri kupitia mapato yake ya ndani kutenga asilimia 10.
Amesema katika bajeti ya 2022/2023 Manispaa ya Morogoro, ilitenga kiasi cha milioni 912,345,060.00 kwa ajili ya mkopo ya uwezeshaji wa kiuchumi kwa Vijana, Wanawake na watu wenye ulemavu.
Katika ujenzi wa madarasa , Mhe. Kihanga, amesema Manispaa imetenga kiasi cha shilingi milioni 625 kwa ajili ya umaliziaji wa maboma 50 ya madarasa ya shule za Msingi.
Katika huduma za afya, Manispaa ya Morogoro imetenga kiasi cha Tshs.300,000,000.00 kwa ajili ya ukamilishaji kituo kimoja cha afya huku ikitenga shilingi milioni 200,000,000.00 kumalizia miundombinu ya Zahanati 4 za Mji Mkuu, Kauzeni, Mafiga na Kihonda.
Mwisho, amewashukuru Viongozi wa vyama vya Siasa, Viongozi wa Taasisi mbalimbali, Waheshimiwa Madiwani , wadau wa maendeleo, Wananchi pamoja na Waandishi wa habari kwa kuhudhuria Mkutano huo muhimu ambapo amesema pamoja na mambo mengine , bajeti hiyo imezingatia Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020 -2025 na mkakati wa kukuza Uchumi na kupunguza Umasikini (MKUKUTA).
Naye Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Ally Machela, amewashukuru Wananchi wote waliohudhuria kikao maalumu cha kupitisha mapendekezo ya mipango ya bajeti 2022/2023.
"Nawashukuru sana Waheshimiwa Madiwani kwa maelekezo yenu ya msingi mliyoyatoa wakati wa kujadili bajaeti hii kupitia kamati zetu za kudumu za Halmashauri, niwapongeze Wananchi wote kupitia Mabaraza ya Maendeleo ya Kata na katika vikao vilivyofanyika katika nyakati na ngazi mbalimbali ,kwa kujitokeza kwa wingi , waandishi wa habari, napenda kuwahakikishia mawazo yenu yamezingatiwa kwa kadri ilivyowezekana katika maandalizi tuliyoyafanya ya bajeti hii” Amesema Machela.
Katika Bajeti ya mwaka 2022/2023 , Halmashauri imelenga kutoa vipaumbele vifuatavyo,Makusanyo ya mapato, elimu , Afya,Usafi wa Mji na utunzaji wa Mazingira, Utawala bora na Mipango Miji.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa