WAZIRI wa TAMISEMI, Mhe. Ummy Mwalimu, amesema kwa sasa Manispaa ya Morogoro ndio Manispaa pekee ambayo itakuwa Chuo Cha kujifunza jinsi ya kuwapanga Machinga.
Kauli hiyo ameitoa Septemba 21/2021 wakati wa uzinduzi wa mabanda ya Machinga Soko Kuu la Chifu Kingalu Morogoro.
Akizungumza na Waandishi wa Habari, Waziri Ummy, amesema moja ya kitu kilichomvutia ni jinsi walivyoweza kupanga vibanda na mfumo bora uliotumika katika kuwaondoa Machinga maeneo yasiyo rasmi na kuwaingiza Sokoni.
"Nimefurahishwa na spidi yenu na utaratibu wenu, nitamke rasmi sasa chuo cha mafunzo ya kuwapanga Machinga kwa Tanzania ni Manispaa ya Morogoro, nipongeze Uongozi wa Mkoa chini ya RC Shigela, Uongozi wa Wilaya chini ya DC Msando, Manispaa ya Morogoro ukiongozwa na Meya wetu Mhe. Kihanga, Mbunge wa Jimbo la Morogoro Mjini Mhe Abdulaziz Abood, Madiwani, wataalamu wa Manispaa pamoja na Machinga kwakweli agizo la Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan mmelitendea haki na mmelifanya kwa haraka na ustadi" Amesema Mhe. Ummy.
Aidha, amewataka Viongozi kuendelea kutatua changamoto nyingine kwani sio Machinga wote ambao wataenea katika Soko hilo.
" Hapa mmejipanga vizuri, angalieni na maeneo mengine ambayo mnaweza kuyapanga kama hivi, wapo Machinga wengi wanaibuka mtaani hivyo mkiwa Viongozi wajibu wenu kuona hao nao mnawajengea mazingira rafiki ya kufanya biashara zao" Ameongeza Waziri Ummy.
Waziri Ummy,amewataka Machinga kuendelea kuwasikiliza Viongozi wao kwani Serikali ipo bega kwa bega na wao kwa kutambua kundi hilo lina mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa Taifa.
Katika hatua nyingine, Waziri Ummy, amesema Serikali ipo katika hatua za mwisho kukamilisha mchakato wa kuwa na Idara pekee itakayoshughulikia biashara, Viwanda na uwekezaji pamoja na Dawati la kushughulikia changamoto za Machinga.
Kwa upande wa Waziri wa Viwanda na Biashara, Prof. Kitila Mkumbo, ameupongeza Uongozi wa Mkoa wa Morogoro kwa maamuzi sahihi ya kuwapanga Machinga katika maeneo rafiki.
Prof. Kitila, amesema Serikali kupitia Ilani ya CCM imeweka mpango wa kutoa ajira zaidi ya Milioni 800 hivyo kuwawezesha Machinga ni njia ambayo ajira zitazalishwa kwa wingi.
" Tukiwa na Machinga sehemu moja, tutakuwa na bodaboda, bajaji ambao watakuwa wanatoa huduma eneo hilo, kwa maana hiyo ajira zitaongezeka na ajira hizi sisemei ajira za vyeti nazungumzia ajira za mzunguko katika biashara " Amesema Prof. Kitila.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe Martine Shigela, amesema chini ya uongozi wake atahakikisha Machinga wanaendelea kusimamiwa vyema kwani wao wanahaki kama ilivyo watu wengine.
" Serikali imewatambua Kama kundi muhimu, hivyo wajibu wetu Viongozi kuwasimamia na kutatua changamoto zao" Amesema RC Shigela.
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe Albert Msando, amesema lengo lake ni kuona Machinga hawawi tena katika kundi la ziada kama ilivyozoeleka.
" Machinga wamekuwa wakichukuliwa Kama kundi la ziada lakini kwa Sasa tumewatambua na tumewahakikishia maisha marefu katika Soko hili ili waendelee kujitafutia riziki" Amesema DC Msando.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro, Mhe Pascal Kihanga, amesema Manispaa ya Morogoro itaendelea kuwalinda Machinga na kuwatafutia maeneo rafiki ya kufanyia kazi.
Mbunge wa Jimbo la Morogoro Mjini Mhe Abdulaziz Abood, amesema watahakikisha wanatengeneza mifumo rafiki ya kuhakikisha Machinga hao wa Soko Kuu la Chifu Kingalu biashara zao zinafanyika na wanapata faida.
Vibanda hivyo vipo 780 kwa Mpango wa awali ambapo idadi kamili inatakiwa kuwa 1000 huku kila kibanda kikigharimu kiasi Cha Shilingi 230,000/=.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa