BARAZA la madiwani la halmashauri ya Manispaa ya Morogoro limeadhimia azimio la kuwafikisha mahakamani wafanyabiashara wakubwa na wa kati waliogomea kwa muda mrefu kulipa jumla ya kiasi cha fedha inayokadiriwa kufikia Sh bilioni 2.1 zinazotokana na kodi ya ushuru wa huduma ( Service Levy ) iliyopo kisheria.
Wafanyabiashara hao wamegoma kulipa kodi ya ushuru wa asilimia 0.3 iliyopitishwa na Bazara Madiwani kwenye vikao vyake vilivyopita, huku wakishinikiza kuwa tayari kulipa kwa kiwango cha asilimia 0.1, kinyume na maamuzi yaliyopitishwa na Baraza la Madiwani.
Azimio la kuwafikisha mahakamani wafanyabiashara hao lilipitishwa katika kikao cha kawaida cha baraza la Madiwani kilichofanyika hivi karibuni baada ya Mkurugenzi wa Manispaa John Mgagula, kuwasilisha taarifa ya mwenendo usio wa kulidhisha wa ukusanyaji wa mapato.
Katika taarifa yake kwa Baraza hilo alisema wafanyabishara wakubwa wanadaiwa kiasi cha Sh bilioni 1.7 na wamegoma kutolipa kodi kwa kiwango cha asilimia 0.3 huku wenyewe wakitaka walipe kiwango cha asilimia 0.1 ambao Ofisi yake imekataa hoja hiyo.
“ Sasa hivi kuna mgomo wa wafanyabiashara wakubwa na wakati , hawataki kulipa kiwango cha ushuru wa huduma cha asilimia 0.3 kilichopitishwa na baraza hili, wamegoma na wamesema wako tayari kulipa asilimia 0.1” alisema Mgalula na kuongeza.
“ Mimi kama Mkurugenzi wa Manispaa kiwango hicho hakiwezi kupunguza ,nina leta kwako Mstahiki Meya ili baraza lako lilidhie twende mahakamani kuwashitaki ” alisema Mgalula.
Nao baadhi ya Madiwani wa baraza hilo, Mabula Lusewa kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA ) alisema kuwa Katibu wa Baraza ambaye ni Mkurugezi amelileta kwetu kutuomba kuruhusu kwenda mahakakani na jambo hilo ni budi lipewe baraka kama tunahuitaji mapato kwa maendeleo yetu sote.
Hata hivyo baadhi ya madiwani Juma Tembo , Mudhihir Shoo na Amir Nondo kwa nyakati tofauti walisema suala hilo linahitaji busara zaidi , kabla ya kuchukua uamuzi wa kwenda mahakamani.
Pamoja na hoja hizo, Mkuu wa wilaya ya Morogoro, Regina Chonjo ambaye alialikwa katika Baraza hilo alisema , Serikali ya Wilaya inaona uamuzi uliochukuliwa na baraza la madiwani kwenda mahakamani uko sahihi, kwani jambo hilo lipo kisheria kutokana na halmashauri kutoza asilimia 0.3 na si zaidi ya hapo .
“ Nikiwa natakiwa nisimamie maendeleo ya Manispaa hii, haiingii akilini jambo lipo kisheria bado linajadiliwa , sheria inawataka walipe kuanzia asilimia 0.1 hadi kufikia 0.3 na si zaidi ya hapo na Baraza hili lilipitisha azimio wafanyabiashara walipe asilimia 0.3 baada ya kufanyika utafiti na wataalamu “ alisema Chonjo.
Hivyo aliunga mkono azimio la kuwafikisha mahakamani wafanyabiashara hao na kushauri kuwa endapo mfanyabiashara mmoja mmoja anayo malalamiko yake ni vyema ayawasilishe kwenye mamlaka za Manispaa ili yafanyiwe kazi na si kuchukua uamuzi wa kugoma kwa kuwa wengi wao wanalipa bila matatizo kodi ya Mamkala ya Mapato Tanzania (TRA).
Kufuatia hoja hizo , Meya wa Manispaa , Pascal Kihanga aliwahoji madiwani hao juu ya azimio la kuwafikisha mahakamani , na wote kwa kauli moja walipitisha azimio hilo la kuwafungulia kesi wafanyabiashara wote wakubwa na wa kati waliogoma kulipa kodi ya huduma wa asilimia 0.3 ulioweka kisheria.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa