MSTAHIKI Meya wa Manispaa ya Morogoro, Mheshimiwa Pascal Mwendishule Kihanga, amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa fedha ambazo Serikali imekuwa ikizileta kwenye Manispaa hiyo na kufanikisha utekelezaji wa shughuli za maendeleo katika sekta mbalimbali ikiwemo sekta za Afya, Elimu Msingi na Sekondari.
Mstahiki Meya Kihanga ametoa shukurani hizo wakati alipokuwa akihutubu katika Mkutano wa Kawaida wa Mwaka wa Baraza la Waheshimiwa Madiwani wa Manispaa ya Morogoro ambapo ameeleza kwamba katika mwaka huu wa fedha 2022/2023, Manispaa imekusanya jumla ya shilingi 80,823,086,209.00 kutoka Serikali Kuu na katika mapato yake ya ndani kwa ajili ya shughuli za uendeshaji wa Halmashauri na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
“Mpaka hivi leo, kutoka Mapato ya Ndani, Manispaa imekusanya jumla ya shilingi 12,653,562,636.00 sawa na asilimia 100 ya makisio ya mwaka, huku shilingi 68,169,523,572.00 zikiwa zimepokelewa kutoka Serikali Kuu,” alifafanua Mstahiki Meya Kihanga.
Aidha, katika hotuba hiyo Mstahiki Meya Kihanga amebainisha mafanikio ya kisekta ambayo Manispaa imeyapata kutokana na makusanyo ya fedha hizo ikiwemo kuanza kwa ujenzi wa Hospitali ya Wilaya katika kata ya Kihonda, ujenzi wa wodi ya wazazi katika Zahanati ya Konga, ujenzi wa Kituo cha Afya katika kata ya Tungi, ujenzi wa zahanati nne katika maeneo ya Uwanja wa Taifa, Mazinmbu,Mlapakolo na Kiegea.
Vilevile, Manispaa imefanikiwa kujenga majengo saba ya utawala katika shule za sekondari Mazimbu, Mbuyni Modern, Kola, Mkundi Mlimani, Mwembesongo, Mafiga na Tungi, ujenzi wa maabara za Sayansi, ujenzi wa mabweni katika shule za sekondari, ujenzi na ukarabati wa vyumba vya madarasa katika shule za msingi na sekondari, ujenzi wa matundu ya vyoo katika shule za msingi na ujenzi wa shule tano mpya za msingi zikiwemo shule za Jitegemee na Kihonda Maghorofani, na ujenzi wa jengo la machinga katika eneo la Fire.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Morogoro, Mheshimiwa Fikiri Juma amelipongeza Baraza la Waheshimiwa Madiwani wa Manispaa ya Morogoro kwa kushirikiana vyema na Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa hiyo pamoja na Menejimenti yake katika kutekeleza shughuli za maendeleo zenye lengo la kutoa huduma bora kwa jamii kulingana na Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na kwa kauzingatia sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma na Serikali kwa ujumla.
“Ombi langu ni kwamba muongeze juhudi katika kutekeleza mpango wa kuendeleza eneo la biashara katikati ya mji (CBD), ili kuwa na matumizi bora ya ardhi katika maeneo ya mjini kwa kuwa mpango huu unahamasisha ujenzi wa maghorofa badala ya ujenzi wa majengo ya chini.”
Mkutano wa Kawaida wa Mwaka wa Baraza la Waheshimiwa Madiwani wa Manispaa ya Morogoro umefanyika tarehe 30.06.2023 katika ukumbi wa mikutano wa Manispaa hiyo.
MWISHO
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa