MANISPAA ya Morogoro imekutanisha wadau mbalimbali wa maendeleo kwenye mdahalo wa ukusanyaji wa maoni ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025-2050 uliofanyika Ukumbi wa Ofisi Kuu ya Manispaa Julai 23-2024.
Imeelezwa kuwa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 imeweza kwa kiasi kikubwa kusogeza mbele maendeleo ya nchi katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu, huduma za afya, miundombinu, maji pamoja na maendeleo ya kiuchumi licha ya changamoto mbalimbali ikiwemo Covid 19 ambayo imesababisha kuchelewa kwa baadhi ya mipango.
Katika ufunguzi wa mdahalo huo Ndg.Hillary Sagara , ambae alimwakirisha Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Rebeca Nsemwa, amesisitiza Viongozi mbalimbali wa Wilaya ya Morogoro walioshiriki kikao hicho kushirikisha wadau mbalimbali kwenye mchakato wa maandalizi ya Dira hiyo ili kupata maoni yatakayo isaidia nchi katika kukua zaidi kiuchumi.
Naye mwenyekiti wa mdahalo huo Ndg.Bakari Msulwa, amesema Dira ya Maendeleo 2025 ilianza kutekelezwa mwaka 2000 na utekelezaji wake utakamilika 2025 na tunatarajia kuanza kutekeleza Dira nyingine ya mwaka 2025-2050 lengo likiwa ni kuiwezesha nchi kuingia katika kundi la nchi za uchumi wa kati.
Aidha ameeleza kuwa kwa ushirikishwaji mpana wa wadau mbalimbali katika maandalizi ya Dira ya maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025-20250 utawezesha kupata Dira jumuishi yenye kukidhi mahitaji stahiki ya Taifa kwa kipindi cha miaka 25 ijayo.
Amesema, Dira ya 2025 pia ilitazamia kuwa na Taifa lenye sifa kuu tano ambazo ni Maisha bora na mazuri,kuwepo kwa amani,utulivu na umoja,uongozi bora na utawala wa kisheria,jamii iliyoelimika na inayopenda kujifunza Zaidi na uchumi imara wenye uwezo wa ushindani ili kukabiliana na nchi nyingine.
Pia, Msulwa, ameongeza kuwa dira ya maendeleo ya Taifa ina gusa makundi yote, hivyo anatarajia ushirikishwaji mpana wa wadau wote katika ngazi zote zikiwemo taasisi za elimu, sekta binafsi, asasi za kiraia na mwananchi mmoja mmoja.
“ Lengo la kujadili mpango wa maendeleo ya dira ya Taifa ya miaka 25 iliyopita na miaka 25 ijayo ni kuimarisha uwezo wa uchumi uliopo na kulinda mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025” Amesema Msulwa.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro, Mhe. Pascal Kihanga, amesema kwa kushirikiana na Baraza la Madiwani na Menejimenti ya Manispaa ya Morogoro watahakikisha kuwa wanatoa elimu kwa wafanyakazi pamoja na wa wanafunzi wa Chuo vyuo ili waweze kutoa maoni kuhusu Dira ya taifa 2050.
Kihanga,amesema kuwa , Dira ya maendeleo 2025 imeisaidia sekta ya elimu kukuwa ikiwemo upatikanaji wa mikopo kwa vyuo vya kati ambayo imewasaidia wanafunzi kujiendeleza kielimu na kuwaondolea wazazi mzigo wa ada kwa watoto wao.
Kwa upande wa mshiriki, Rubben Rashid, amesema miaka 25 ijayo ya mpango wa maendeleo, Serikali ijikite katika utoaji wa elimu yenye kumfanya mwanafunzi kujiajiri badala ya kuajiriwa.
Naye Mwenyekiti wa Chama Cha CHAUMA Manispaa ya Morogoro, Ismail Rashid, amesema ili mpango huo wa maendeleo ya Taifa ufanikiwe, lazima viongozi waongeze kasi ya uwajibikaji na utawala bora.
Naye mwanafunzi wa darasa la 7 shule ya Msingi Mwere A , Seaba Mbega , ameomba vifaa vya TEHAMA Mashuleni vipelekwe ili kurahisisha wanafunzi kujifunza kwa vitendo somo hilo kuanzia shule za msingi.
Pia mwanafunzi Elizabeth Jackson kutoka shule ya Msingi Mwere A, amesomba huduma za afya ziboreshwe kwani bado kuna changamoto kwenye sekta hiyo hususani kwa wamama wajawazito na madirisha ya wazee.
Aidha Mwenyekiti wa chama cha watu wenye Uhalbino Mkoa wa Morogoro(TAS) Hassan Mikazi amesema Dira ya 2050 izingatie watu wenye ulemavu hasa katika Nyanja zote za kielimu,kiuchumi kiafya, miundombinu na kisiasa.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa