MKUU wa Mkoa wa Morogoro,Mhe. Adam Malima, amefanya ziara ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo katika Manispaa ya Morogoro lengo ikiwa ni kuangalia namna miradi hiyo inatekelezwa huku akielezea namna ambavyo amefurahishwa na utekelezaji wa miradi hiyo.
Akiongea katika ziara hiyo iliyofanyika Juni 22/2023,RC Malima , ameipongeza Manispaa ya Morogoro, kwa utekelezaji wa miradi hiyo na kwa jinsi wanavyoshirikiana vyema baina ya viongozi wa Serikali na wa chama katika kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa ipaswavyo.
Aidha RC Malima , amesema ofisi yake itafanyia kazi maoni ya wananchi pamoja na viongozi ikiwa ni lengo la kuufanya Mkoa wa Morogoro kuwa na maendeleo makubwa .
RC Malima , amesema amefurahishwa na ushirikiano alioupata wakati wa ukaguzi wa miradi hiyo na amewataka watumishi wa Serikali na viongozi wote wa Manispaa kuendelea kushirikiana na kuwasisitiza kusimamia vyema ukusanyaji wa mapato.
Pia RC Malima, amesisitiza viongozi wote wa Manispaa kufanya ufuatiliaji wa shughuli za miradi, kusikiliza na kutatua kero za wananchi, kuendelea kusimamia usafi wa mazingira, kuendelea kuyalinda maeneo ambayo machinga wameondolewa.
Kuhusu kupata eneo la ujenzi wa shule nyengine mpya ya Sekondari Kata ya Mkundi, RC Malima, amemuagiza Mkurugenzi kuandika barua ya maombi kwa Wilaya ya Mvomero ili kuona namna ya kupata eneo la CCT ambalo wamekuwa wakitamani shule kujengwa katika eneo hilo.
Katika kuhakikisha huduma ya maji inakuwa ya kutosha, amesema atakutana na Waziri wa Maji Mhe.Juma Aweso, kuona namna ya kuharakisha huduma hiyo kwani imekuwa ni kero kwa wananchi ambao wamekuwa na matumaini makubwa na Serikali yao ya Awamu ya Sita chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Morogoro Mjini, amewataka Madiwani kuendelea kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Kata zao ili wananchi ambao walipakodi wafaidi matunda ya kodi zao.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Rebeca Nsemwa, amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa ziara yake na kuahidi kuwa maelekezo yote aliyoyatoa yatafanyiwa kazi na kutekelezwa ipaswavyo na kuhakikisha Wilaya ya Morogoro inaendelea kuwa ya mfano kwa nyanja zote.
Katika ziara hiyo , miongoni mwa miradi iliyotembelewa ni Ujenzi wa Shule mpya ya mfano ya Ghorofa iliyopo Kata ya Boma, Kituo cha afya Tungi, Uzinduzi wa Jengo la Utawala Shule ya Sekondari Mkundi Mlimani pamoja na Kituo cha Afya Lukobe.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa