HALMASHAURI ya Manispaa ya Morogoro katika kipindi cha mwaka 2017/2018 imetoa mkopo wa kiasi cha shilingi milioni 113,500,000.000 kwa vikundi 70 vya wanawake kwa lengo la kuwawezesha kiuchumi.
Mkopo huo ulitolewa kwa lengo la kuwaongezea mtaji wajasiriamali ili kuweza kukuza biashara zao na kuzalisha kwa wingi na hatimaye kuendana na Agizo la Mh.Rais Dkt.Magufuli la kuwa na Tanzania ya viwanda katika kukuza uchumi wa Taifa.
Hayo yaliainishwa na Afisa Maendeleo na Ustawi wa Jamii,Enedy Mwanakatwe katika maadhimisho ya siku ya wanawake duniani yaliyofanyika katika viwanja vya shule ya msingi Kiwanja cha Ndege.
Mwanakatwe alisema kuwa halmashauri inaendelea kuwajengea vijana uwezo wa kujitambua,kuwa wabunifu na kuanzisha viwanda vidogo vidogo,lengo ni kuhakikisha kila kijana anajituma kuzalisha na kuepuka kukaa vijiweni.
“Vikundi 34 vya vijana vimepitishwa na mabaraza ya maendeleo ya kata kwa ajili ya kupewa mikopo mwezi Aprili,2018 na tunarajia kuwapa kiasi cha shilingi milioni 102,000,00.00.”Alisema Mwanakatwe.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Morogoro Mjini,Aziz Abood alisema kuwa ni wakati sasa wanawake kutumia fursa zilizopo katika jamii na kuweza kuzalisha na kuondokana na hali ya kuwa tegemezi ndani ya familia zao.
Abood alisema ndani ya manispaa ya Morogoro kuna vikundi vingi vya ujasiriamali hivyo kila mwanamke kuhakikisha anajiunga katika kikundi kimojawapo ili kuweza kusonga mbele,kwani hakuna mtu anaweza kufanikiwa bila kuwa na ushirikiano na wenzake.
“Naomba sana wanawake tujiunge katika vikoba,tushiriki mafunzo mbalimbali ya ujasiriamali ili tuweze kuzalisha wenyewe katika viwanda vidogo vidogo na kuendana na kasi ya sera ya Tanzania ya viwanda.”Alisema Abood.
Alisema kuwa ataendelea kushirikiana na halmashauri ya manispaa ya Morogoro kuhakikisha vikundi vyote vilivyosajiliwa na kutambulika vinasonga mbele na kuweza kupatiwa fedha za kuendesha kikundi hicho.
Aidha Mkuu wa Wilaya ya Morogoro,Regina Chonjo aliwataka wanawake kuwa mstari wa mbele kutoa taarifa za vitendo vya ukatili wa kijinsia wanavyofanyiwa ndani ya jamii ili kuweza kutokomeza janga hilo.
Chonjo alisema kuwa wanawake ndio tegemezi katika sakata zima la uzalishaji ndani ya familia,hivyo hatuwezi kufikia Tanzania ya viwanda kama mwanamke ataendelea kunyanyaswa na kufanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa