MANISPAA ya Morogoro imezindua rasmi mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma kwa Shule za Msingi Tanzania (UMITASHUMTA).
Uzinduzi huo umefanyika Mei 10/2023 kwenye viwanja vya shule ya Morogoro Sekondari Kata ya Boma kwa kuwashirikisha wanamichezo kutoka shule zote za Msingi ndani ya Manispaa hiyo zilizogawanywa kikanda, Kanda ya Mashariki, Magharibi, Kusini na Kaskazini na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa vyama vya michezo pamoja na walimu kutoka shule hizo.
Akifungua mashindano hayo , Afisa Elimu Taaluma Msingi Manispaa ya Morogoro, Bi. Aneth Fundi, akimwakilisha Mkurugenzi wa manispaa ya Morogoro, amesema kuwa lengo kubwa la mashindano hayo ni kuunda timu kubwa ya Halmashauri itakayowezesha kuleta ushindani pamoja na kuibua vipaji vya watoto Shuleni.
“leo ndio tunafungua rasmi mashindano haya na lengo kubwa la mashindano hayo ni kuunda timu kubwa na bora katika Halmashauri yetu kwenye michezo yote kwahiyo ombi langu kwenu, kila mmoja ashiriki kikamilifu katika eneo alilopangiwa ili tuweze kupata timu bora ya Manispaa ambayo itaenda kutuwakilisha vizuri kwenye mashindano ya Mkoa, hivyo amewaomba Vijana kucheza kwa upando kwani michezo ni afya na ni ajira pia" Amesema Bi. Aneth.
Aidha,Bi. Aneth, amewaasa walimu waliopewa dhamana ya kuunda timu ya Manispaa kuacha kuchagua wanamichezo kwa upendeleo.
“Niwasihi walimu mliopewa dhamana ya kuunda timu ya Manispaa kuacha tabia ya kuchukua wanamichezo kwa upendeleo, undeni timu kadri mwanafunzi mwenyewe anavyoonesha kipaji chake katika michezo, ili tupate timu imara katika fani zote na tuweze kushiriki kimkoa na hata kitaifa” Ameongeza Bi. Aneth.
Pia wanamichezo hao ambao ni wanafunzi kutoka shule mbalimbali za Msingi ndani ya Manispaa hiyo wametakiwa kuhakikisha kwamba wanakuwa na nidhamu na kujituma katika eneo walilopangiwa katika kipindi chote cha michuano hiyo ili wawe miongoni mwa watakao unda timu ya Manispaa badae kimkoa na kufika kitaifa.
Kwa upande wa Afisa Michezo Manispaa ya Morogoro, Asteria Mwang'ombe, amewataka Waalimu wa michezo Manispaa ya Morogoro kutumia michezo ya UMITASHUMTA kuibua vipaji kupitia hazina ya Vijana wadogo waliopo katika shule za Msingi wenye uwezo mkubwa katika michezo mbalimbali.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa