MANISPAA ya Morogoro imejipanga kukabiliana na Mvua za El- Nino zinazotarajiwa kuanza hivi karibuni kwa kutenga Milioni 30 kwa ajili ya kutatua changamoto zitakazowakumba wahanga.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, ndugu Ally Machela, mara baada ya kumalizika kwa Baraza la Kawaida la Waheshimiwa Madiwani la robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2023/2024 kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Manispaa hiyo.
Ndugu Machela amesema kuwa elimu tayari imeshatolewa katika maeneo yenye viashiria vya mafuriko na wananchi zaidi ya 130 wameshajitokeza kuhitaji viwanja mbadala ili kuepukana na athari za mafuriko zinazoweza kujitokeza.
"Tayari timu yetu imeshapita mitaani kutoa elimu, lakini pia tuliwaomba wananchi wahame kwenye maeneo yanayoweza kuathirika, na tumepokea maombi ya wananchi 130 ambao tunatarajia kuwapatia viwanja maeneo ya Kiegea kwa ajili ya kujenga nyumba zao kwa bei nafuu ya skwea mita 1 kwa shilingi 3500" Amesema Machela.
Vilevile, ndugu Machela amesema kwa kutumia eskaveta ya Manispaa wamejipanga kuanza kusafisha mitaro na mifereji yote katika maeneo yenye viashiria vya mafuriko kwa lengo la kuokoa na kupunguza maafa yanayoweza kujitokeza hapo baadae.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa