Asubuhi tarehe 28.04.2024, Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Morogoro ndugu Emmanuel Mkongo, amemkabidhi Mwenge wa Uhuru pamoja na wakimbizaii wa kimkoa na wa kitaifa, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Morogoro ndugu JoanFaith Katalaiya.
Awali alipokuwa akizungumza na umma uliokuweo wakati wa makabidhiano hayo, ndugu Mkongo amesema jana asubuhi Mwenge wa Uhuru ulipowasili kwenye Manispaa ya Morogoro, ulikimbizwa umbali wa kilomita 94, kwenye miradi 10 ya maendeleo , yenye thamani ya shilingi bilioni 3.6, ambazo ni fedha kutoka Serikali Kuu, Mapato ya Ndani ya Manispaa na michango ya wananchi wa Manispaa ya Morogoro.
“Katika miradi kumi iliyopitiwa na Mwenge wa Uhuru, mitano ilionwa, miwili iliwekewa jiwe la msingj kila mmoja, na miwili ilizinduliwa” alifafanua Mkongo.
Kwa upande wake Mkufunzi wa Mwenge wa Uhuru Kitaifa Kapten Musa Mohamed Ngomambo amempongeza mbunge wa jimbo la Morogoro Mjini Mheshimiwa Dkt. Abdul-Aziz Abood pamoja na mbunge wa viti maalumu wa jimbo hilo Mheshimiwa Dkt. Christine Ishengoma kwa kushiriki kikamilifu katika Mapokezi na safari nzima ya kuukimbiza Mwenge wa Uhuru mpaka kuukabidhi kwenye jimbo la Morogoro Vijijini.
Kapten Ngomambo amesema kuwepo kwa wabunge hao kwenye mbio za Mwenge wa Uhuru ndani ya Manispaa ni faraja kubwa kwake na wenzake, kwa sababu waheshimiwa wabunge ndio ambao huisemea bungeni miradi ya maendeleo ambayo hutekelezwa na Halmashauri kwenye majimbo yao.
Naye Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa (2024) ndugu Godfrey Mnzava ameipongeza Manispaa ya Morogoro kwa kuwa na Mapokezi mazuri ya Mwenge wa Uhuru, an miradi mizuri ya maendeleo ambayo Mwenge wa Uhuru imeitembelea.
Ndugu Mnzava ameitaka Manispaa ya Morogoro kuendelea kusimamia miradi ya maendeleo na kuhakikisha inaleta tija kwa wananchi wa Manispaa hiyo.
Miongoni mwa miradi ya maendeleo iliyopitiwa na Mwenge wa Uhuru kwenye Manispaa ya Morogoro ni pamoja na mradi wa Zahanati ya Kauzeni kata Kauzeni, mradi wa upandaji wa miti kata Mindu, mradi wa jengo la wafanya biashara wadogo (machinga) kata ya Uwanja wa Taifa, miradi miwili ya maji, mradi wa kikundi cha vijana wanufaika wa mkopo wa asiimia kumi, na mradi wa ujenzi wa barabara ya zege ya Kichangani.
MWISHO
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa