Kamati ya Fedha na Uongozi ya Halmashauri ya Jiji la Tanga, ikiongozwa na mwenyekiti wake, ambaye pia ndiye Mstahiki Meya wa Jiji hilo, Mheshimiwa AbdulRahman Omary Shiloow, pamoja na baadhi ya wataalamu kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Jiji hilo, wameitembelea Manispaa ya Morogoro kwa lengo la kujifunza uendeshaji wa kitega uchumi cha stendi ya mabasi ya Msamvu inayokadiriwa kuiingizia Manispaa mapato ya zaidi ya shilingi bilioni mbili kila mwaka.
Akizingumza na wakuu wa vitengo na divisheni za Manispaa ya Morogoro, katika kikao kilichotangulia kabla ya kamati hiyo kuzuru stendi ya Msamvu, Mheshimiwa Shiloow alisema Jiji la Tanga linacho kitega uchumi ambacho kwa sasa ujenzi wake umefikia asilimia 97 hivyo wao kama Kamati ya Fedha na Uongozi wanatamani kuona kitega uchumi hicho kikiimarisha zaidi mapato ya Jiji lao pindi kitakapoanza kufanya kazi.
“Japokuwa kuna msemo usemao kwamba sikio haliwezi kuzidi kichwa, sisi kwa ziara hii, tunategemea tutaweza kwenda kuweka namna bora zaidi ya uendeshaji wa kitega uchumi chetu kwani mwanafunzi hanabudi kufanya vizuri zaidi ya mwalimu wake, na Manispaa ya Morogoro mmekuwa mwalimu mzuri kwetu ndio maana awamu ya kwanza kuna wenzetu walikuja kujifunza na sisi leo tumerudi ili kukazia maarifa” alieleza Mheshimiwa Shiloow.
Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro, Mheshimiwa Pascal Kihanga, amemshukuru Mstahiki Meya wa Jiji la Tanga pamoja na timu yake kwa kuichagua Manispaa ya Morogoro kuwa sehemu ya wao kuja kujifunza jinsi ya kuendesha kitega uchumi chao.
“Ninamshukuru Mungu kwamba Manispaa hii ya Morogoro imekuwa chuo cha mafunzo kwani Halmashauri kadhaa zimekuwa zikija kujifunza mambo mbalimbali kutoka hapa na ni imani yangu kwamba nanyi mkishajifunza leo, mtafanya vizuri zaidi” alisema Mheshimiwa Kihanga.
Aidha, wakiwa kwenye kituo cha Mabasi cha Msamvu, wanakamati hao kutoka Jiji la Tanga walipata fursa ya kusikiliza taarifa ya uendeshaji wa kitega uchumi hicho, kutoka kwa meneja wake, wakaona jinsi mifumo ya kielektronki inavyotumika kufuatilia kila kitu kinachotendeka ndani ya kitega uchumi, sambamba na kuona jinsi ukusanyaji wa mapato unavyosimamiwa katika maeneo yote ya kuingilia na ya kutokea.
Stendi ya Mabasi ya Msamvu ni miongoni mwa vitega uchumi vikubwa vya Manispaa ya Morogoro tangu mwaka 2018 ilipokabidhiwa rasmi kwa Manispaa, kutoka mikononi mwa mmliki wa awali, aliyejulikana kama Msamvu Property.
MWISHO
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa